Habari Mseto

Faini ya Sh440,000 kwa kubugia pombe wakati usiofaa

July 25th, 2019 1 min read

Na MWANGI MUIRURI

WATU 11 walitozwa faini ya Sh440,000 na mahakama ya Kaunti ya Murang’a baada ya kukiri kushiriki biashara ya pombe kinyume na saa zilizowekwa kwa mujibu wa sheria.

Walikamatwa mapema asubuhi wakiuzia walevi pombe, ambapo walevi hao wakiamka asubuhi, husingizia kuwa hawawezi wakatekeleza lolote la kimaisha kabla ya kubugia pombe.

Washukiwa hao walishtakiwa chini ya msako mkali unaoendelezwa katika Kaunti hiyo ya Murang’a kutokana na kuripotiwa wanaume wawili kuaga dunia katika mtaa wa Gakoigo mwishoni mwa wiki iliyopita.

Washukiwa hawa walijumuisha wahudumu wanane wa kike na wawili wa kiume na ambao walifikishwa mbele ya hakimu Joseph Gathuku wa mahakama ya Kigumo.

Wote walikiri makosa hayo na Hakimu Gathuku akawatunuku adhabu ya faini ya Sh40, 000 kwa kila mmoja au wahudumu kifungo cha miezi sita gerezani.

“Mlikamatwa kihalali na mmeshtakiwa kihalali. Mmekiri makosa kama mlivyosomewa na mahakama hii haina budi kuwatunuku adhabu kwa mujibu wa sheria zilizoko,” akasema.