MakalaSiasa

Faini za kushindwa kutetea kesi za uchaguzi kortini zatisha wengi

February 12th, 2018 3 min read

Bi Wavinya Ndeti aliyewasilisha kesi mahakamani kupinga ushindi wa Gavana wa Machakos Dkt Alfred Mutua. Bi Ndeti alipoteza kesi hiyo. Jaji Aggrey Muchelule alimwagiza kulipa Sh10 milioni ambazo zitagawanywa kati ya Dkt Mutua na IEBC. Picha/ Maktaba

Na JEREMIAH KIPLANG’AT na VALENTINE OBARA

Kwa Muhtasari:

  • Jumla ya kesi 277 za kupinga matokeo ya uchaguzi mbalimbali ziliwasilishwa mahakamani
  • Kuna hatari ya maamuzi ya aina hiyo kufanya watu maskini ambao hawana misingi thabiti ya kuwasilisha kesi wasifanye hivyo kwa hofu ya kubebeshwa mzigo wa mamilioni ya pesa
  • Kwa kuamua gharama ya kesi, majaji huzingatia aina ya ushahidi uliowasilishwa na kiwango cha wakati kitakachotumiwa katika kesi nzima
  • Ili kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais mlalamishi anahitajika kuweka ada ya Sh1 milioni

WANASIASA ambao kesi zao za kupinga matokeo ya uchaguzi zilitupwa nje wanakumbwa na gharama kubwa ya malipo wanayoagizwa kulipa na majaji mbali na ada nyingine za kesi na malipo ya mawakili wao.

Kufikia sasa, gharama kubwa zaidi nchini ilikuwa kwa Katibu Mkuu wa Chama cha KANU, Bw Nich Salat, ambaye aliagizwa kulipa Sh67 milioni kwa jumla.

Miongoni mwa pesa hizo ni Sh57.6 milioni alizohitajika kumlipa aliyekuwa Seneta wa Kaunti ya Bomet, Bw Wilfred Lesan, na Sh 10.4 milioni kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Jumla ya kesi 277 za kupinga matokeo ya uchaguzi mbalimbali zilikuwa zimewasilishwa mahakamani kufikia Septemba 8, ambayo ndiyo ilikuwa siku ya mwisho kuwasilisha kesi hizo. Idadi hii ni ongezeko la asilimia 89 ikilinganishwa na kesi 188 zilizowasilishwa baada ya uchaguzi wa mwaka wa 2013.

Inaaminika ongezeko hilo lilitokana na uamuzi wa Mahakama ya Juu mnamo Septemba 1, wa kufutilia mbali ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta, baada ya uchaguzi wa Agosti 8.

Kulingana na wakili Robinson Kigen, ambaye amewahi kusimamia kesi za uchaguzi, inaonekana mahakama zinawasilisha ujumbe kwamba hazitaruhusu watu watumie mahakama vibaya kwa kuwasilisha kesi zisizo na msingi.

 

Watu maskini

Hata hivyo, aliongeza kuwa kuna hatari ya maamuzi ya aina hiyo kufanya watu maskini ambao hawana misingi thabiti ya kuwasilisha kesi wasifanye hivyo kwa hofu ya kubebeshwa mzigo wa mamilioni ya pesa.

“Huenda tukafanya kuwe na hali ambapo malalamishi yatakuwa yameachiwa tu matajiri katika jamii kwani wao pekee ndio watakuwa na uwezo wa kugharamia ada ghali ya kesi za uchaguzi,” akasema.

Kesi ya karibuni zaidi ambayo imegonga vichwa vya habari ni ile iliyowasilishwa na Bi Wavinya Ndeti, kupinga ushindi wa Gavana wa Machakos, Dkt Alfred Mutua.

Ijumaa iliyopita, Bi Ndeti aliagizwa na Jaji Aggrey Muchelule, kulipa Sh10 milioni ambazo zitagawanywa kati ya Dkt Mutua na IEBC.

Novemba mwaka uliopita, Kiongozi wa Chama cha Narc-Kenya, Bi Martha Karua, pia aliagizwa kulipa Sh10 milioni baada ya kushindwa kwenye kesi ambayo alikuwa amepinga ushindi wa Gavana wa Kirinyaga, Bi Anne Waiguru. Hata hivyo, mbunge huyo wa zamani wa Gichugu alikata rufaa dhidi ya uamuzi uliotolewa na Jaji Lucy Gitari.

 

Waliopinga ushindi wa Sonko na Ongeri

Mapema mwezi uliopita katika Kaunti ya Nairobi, wapigakura Japheth Muroko na Zachaeus Okoth Oliech, waliagizwa na Jaji Msagha Mbogholi kulipa Sh5 milioni, katika kesi ambapo walikuwa wamepinga ushindi wa Gavana Mike Sonko.

Hali sawa na hii ilishuhudiwa Kisii ambapo Jumatatu iliyopita Jaji Winfrida Okwany, aliagiza walalamishi George Ogake na Charles Orito, walipe Sh8 milioni. Walikuwa wamepinga ushindi wa Seneta Sam Ongeri.

Seneta wa Makueni, Bw Mutula Kilonzo Jr, alisema haoni kama ada zinazoamuliwa walalamishi walipe sasa ni za juu kuliko ilivyokuwa miaka iliyotangulia.

“Gharama ya kesi huamuliwa kwa mujibu wa kiwango cha kazi kinachofanywa wakati wa kesi, na muda utakaotumiwa kwenye kesi hiyo. Hakuna sheria inayoongoza uamuzi huu kwa sababu huwa inategemea matukio mahakamani,” akasema seneta huyo ambaye pia ni wakili.

Kwa kuamua gharama ya kesi, majaji huzingatia aina ya ushahidi uliowasilishwa, idadi ya mashahidi watakaoitwa na la muhimu zaidi, kiwango cha wakati kitakachotumiwa katika kesi nzima.

Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa, Bw Philip Chebunet, asema mahakama zinajaribu kuzuia baadhi ya watu kupeleka hasira zao mahakamani wanaposhindwa uchaguzini.

 

Gharama kubwa

“Mahakama zinajaribu kuambia watu ambao huzitumia kutoa hasira zao kwamba itawagharimu sana kufanya hivyo,” akasema Bw Chebunet, ambaye pia ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Eldoret.

Mbali na gharama hizo zinazoamuliwa na majaji, kuna ada nyingine zinazohitajika kulipwa katika kesi za kupinga matokeo ya uchaguzi.

Kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Agosti 8, Jaji Mkuu David Maraga, alichapisha kwenye gazeti rasmi la serikali ada ambazo zingehitajika kulipwa mahakamani kabla ya kesi kuidhinishwa kuendelea. Kulingana naye, ada hizi zilinuia kufanya kuwepo utaratibu laini.

Ili kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais, mlalamishi alihitajika kuweka ada ya Sh1 milioni ya udhamini ambayo angerudishiwa baada ya kesi, na Sh500,000 nyingine ambazo zisingerudishwa.

Waliotaka kupinga matokeo ya uchaguzi wa gavana, seneta au mbunge walihitajika kwanza walipe Sh30,000 ambazo wasingerudishiwa, na Sh100,000 za udhamini ambazo wangerudishiwa iwapo kesi ingefaulu. Kupinga matokeo ya uchaguzi wa diwani kulihitaji ada ya Sh15,000.