Michezo

Faith Kipyegon akosa mshindani wa kumtoa jasho katika mbio za mita 1,500 mjini Ostrava

September 9th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

BINGWA wa Olimpiki katika mbio za mita 1,500 Faith Kipyegon aliendeleza ubabe wake katika ulingo wa riadha kwa kuibuka mshindi mara tatu mfululizo tangu kurejelewa kwa mashindano mbalimbali kalenda ya mbio msimu huu.

Kipyegon, 26, alitamalaki mbio za mita 1,500 kwenye Riadha za Dunia za Continental Gold Tour zilizoandaliwa katika uwanja wa Mestky, mjini Ostrava, Jamhuri ya Czech kwa kusajili muda wa dakika 3:59.05 mnamo Jumanne usiku.

Muda huo wa Kipyegon ulimwezesha kufuta rekodi ya dakika 4:00.96 iliyowekwa na Mwethiopia Gudaf Tsegay katika mbio hizo mnamo 2017.

Mtimkaji huyo aliyempiku Mwingereza Laura Weightman, alisajili muda bora wa dakika 3:59.05 uliomwezesha kuweka rekodi mpya katika makala ya kivumbi cha Ostrava Golden Spike.

Ilikuwa mara ya kwanza kwa Kipyegon kunogesha mbio za mita 1,500 ambayo ni fani aliyoizoea baada ya kutawala mbio za mita 1,000 kwenye duru za Wanda Diamond League zilizoandaliwa mjini Monaco, Ufaransa na Brussels, Ubelgiji.

Katika duru hizo zote za Diamond League, Kipyegon alikuwa pua na mdomo kuvunja rekodi ya dunia ya dakika 2:28.98 iliyowekwa na Mrusi Svetlana Masterkova katika mbio za mita 1,000 mnamo 1996.

Kipyegon alikosa mshindani wa kumtoa jasho mjini Ostrava baada ya kutumia dakika 2:11.84 kufikia hatua ya mita 800 na kukamilisha umbali wa mita 1,200 kwa muda wa dakika 3:15.39 pekee.

Mkenya Sheila Chelagat aliambulia nafasi ya pili kwenye mbio za mita 5,000 nyuma ya Sifan Hassan wa Uholanzi ambaye pia ni bingwa wa dunia katika mbio za mita 10,000 na mita 1,500. Chelagat alisajili muda bora wa binafsi wa dakika 14:40:51, sekunde tatu pekee nyuma ya Hassan (14:37:85).

Kukosekana kwa Mkenya Timothy Cheruiyot ambaye ni bingwa wa dunia katika mbio za mita 1,500, kulimpa Jakob Ingebrigtsen wa Norway fursa ya kutamba katika fani hiyo. Ingebrigtsen alisajili muda wa dakika 3:33:92 na kumpiku chipukizi wa Kenya Kumari Taki aliyeambulia nafasi ya pili kwa dakika 3:34:14.

Katika mbio za mita 800, bingwa wa Jumuiya ya Madola, Wycliffe Kinyamala alitupwa hadi nafasi ya saba kwa muda wa dakika 1:45:53. Mbio hizo za mizunguko miwili zilizotawaliwa na Mwingereza Jake Wightman kwa muda wa dakika 1:44:18, zilikuwa za kwanza kwa Kinyamal kushiriki msimu huu.

Mganda Jacob Kiplimo alisajili muda wa dakika 12:48.63 katika mbio za mita 1,500 kwa upande wa wanaume na kumpiku mshindi wa nishani ya fedha duniani, Selemon Barega wa Ethiopia aliyeridhika na nafasi ya pili.