Familia 100 zilizopoteza nyumba zao katika kisa cha moto South B hazijarudi makwao mwezi mmoja baada ya tukio

Familia 100 zilizopoteza nyumba zao katika kisa cha moto South B hazijarudi makwao mwezi mmoja baada ya tukio

Na SAMMY KIMATU

NAIROBI

ZAIDI ya familia 100 ambazo zilipoteza nyumba na mali wakati wa tukio la moto katika mtaa mmoja wa Mabanda South B mwezi uliopita hawajarudi makwao.

Akizungumza na Taifa Leo jana, chifu wa eneo hilo, Bw Paul Muoki Mulinge alisema wamiliki wa nyumba katika mtaa wa Mukuru-Fuata Nyayo ‘A’ ulioko ndani ya wadi ya Nairobi Kusini wanakabiliwa na shida za kifedha zinazosababishwa na janga la Covid-19.

“Wamiliki hawawezi kujenga upya nyumba zao kwa sababu ya ukosefu wa pesa. Wengi wanadai wana mzigo wa karo ya shule huku shule zikifunguliwa wiki ijayo,” Chifu Mulinge asema.Vilevile, wengine walidai walipoteza kazi na walitegemea kodi kutoka kwa wapangaji ambao walichukua nyumba zao.

Wakati huu, waathiriwa wamepatiwa makazi na watu wa familia, marafiki na majirani katika mitaa ya mabanda jirani.Bw Mulinge ameongeza kuwa serikali imeamuru wamiliki wote wa nyumba zilizochomeka waache nafasi ya barabara ya kutumika wakati wa dharura.

Picha/SAMMY KIMATU
Bw Caleb Njairo, 37 aonyesha mahali mtoto wake wa kike Melvin Ayona wa miaka 7 alifia wakati wa kisa cha moto kilichoua watu wawili mtaa wa mabanda wa Mukuru-Fuata Nyayo South B Nairobi.

“Lazima tuhakikishe utekelezaji wa kuwajibika kuacha barabara za kuingia mtaani kabla ya kujenga nyumba upya ili kuzuia vifo na uharibifu wa mali,” Bw Mulinge akaongeza.Wakati wa kisa hicho, mali ya mamilioni ya pesa iliharibiwa na moto.

Isitoshe, watu wawili walipoteza maisha huku mtu wa tatu akiuguza majeraha ya moto katika hospitali ya rufaa ya Kenyatta.Kamanda wa polisi kaunti ndogo ya Makadara, Bw Timon Odingo alisema moto huo ulisababishwa na mshumaa uliowashwa baada ya mpangaji kulala kabla ya kuuzima.

“Moto ulianza kutoka nyumba moja ambapo mwanamume alikuwa amelala usingizi mzito kabla ya kuzima mshumaa. Moto ulienea kwa kasi hadi nyumba zingine ukipepewa na upepo,” Bw Odingo akanena.

  • Tags

You can share this post!

Afisa Mkuu Mtendaji wa AC Milan, Ivan Gazidis, augua...

Tiketi ya ODM yavutia wengi wanaotaka kurithi Ojaamong