Habari Mseto

Familia 106 zalala nje baada ya nyumba zao kuteketea

September 21st, 2020 1 min read

NA SAMMY KIMATU

[email protected]

Nairobi

ZAIDI ya familia 100 katika mtaa mmoja wa mabanda walikesha nje kwa baridi baada ya moto kuteketeza nyumba zao mwishoni mwa wiki.

Tukio hilo lilitokea Jumamosi jioni katika mtaa wa mabanda wa Mukuru-Fuata Nyayo katika wodi ya Nairobi South iliyoko kaunti ndogo ya Starehe kaunti ya Nairobi.

Mwathiwa, Bi Sarah Wambui, 48 alisema moto ulianza kutoka nyumba mojo kabla ya kuenea haraka na kusambaa kwa nyumba zingine.

Bi Wambui aliongeza kuwa alipoteza mali yake yote iliyokuwa nbdani ya nyumba mbili alizokuwa akiishi wakati wa tukio hilo.

Aisha, shule moja ya kibinafsi karibu na eneo la tukio ilikuwa na bahati baada ya moto kuzuiliwa na ukuta wa mawe.

Bw Isaiah Kinyosi, mwenye umri wa miaka 32 aliiambia Taifa Leo kwamba msongamano wa nyumba ni changamoto nyingine katika kupambana na moto mtaani huo wa mabanda baada ya watu kunyakua ardhi.

Aliwauliza viongozi kuweka mikakati kambambe kuhakikisha barabara za kutumiwa wakati wa dharura zimepatikana

Mwathiriwa mwingine, Bw Samson Tinega, ambaye ni mlinzi mwenye umri wa miaka 42, alinusurika kifo kwa tundu la sindano kwani alikuwa amelala wakati huo.

“Majirani waliniokoa nilipokuwa nikishindwa kupumua kwa sababu ya moshi. Walakini, walivunja mlango nikiwa bado usingizini na kuniokoa nikiwa hai na ninamshukuru Mwenyezi Mungu, ” Bw Tinega akasema.

Wakazi walidai waporaji walijinufaisha wakijifanya kuwa wasamaria wema katika kukurukakara za kuzima moto.

Vijana walitumia maji ya bomba wakati wengine wakibomoa nyumba zingine ili moto usienee zaidi.

Vilevile, mtu mmoja alipelekwa hospitalini baada ya kukatwa na mabati. Polisi wameanzisha uchunguzi kubaini chanzo cha moto.