Habari Mseto

Familia 15 zaokolewa baada ya nyumba ya orofa tatu kuangushwa na mafuriko

April 28th, 2024 2 min read

NA SAMMY KIMATU

FAMILIA 15 zimeponea kifo kwa tundu la sindano baada ya kuokolewa na maafisa wa utawala kabla ya nyumba ya orofa tatu waliyokodi kuporomoka mwishoni mwa juma.

Akiongea Jumapili na Taifa Leo, naibu kamishna wa kaunti ndogo ya Starehe, Bw John Kisang alisema nyumba hiyo, katika mtaa wa mabanda wa Mukuru-Sokoni, South B, ilikuwa na nyufa na pia kuonyesha dalili za kuinama upande mmoja.

Bw Kisang alisema baada ya maafisa wa utawala wakiongozwa na mkuu wa tarafa, Bw Solomon Wangari Muraguri, maafisa wa polisi sawia na wahudumu katika Shirika la Msalaba Mwekundu na wengine kutoka katika serikali ya Kaunti ya Nairobi walifika katika eneo la mkasa kutathmini hali halisi.

“Tulianza shughuli za kuokoa familia zote na kuhakikisha wote wako salama. Lililofuata ni kutoa amri ya nyumba hiyo ibomolewe mara moja,” Bw Kisang akasema.

Aidha, nyumba hiyo, kulingana na mkuu huyo wa Starehe, ajabu ni kwamba ilikuwa imejengwa katika mto Ngong Ngong.

Mkuu wa polisi katika eneo la Makadara, aliangiza maafisa wake kuwa chonjo katika eneo hilo kuhakikisha wapangaji wote wamo salama pamoja na mali yao wakati wa zoezi nzima ya kuondoa bidhaa zao kuhamia kwingineko.

“Mbali na kuhakikisha usalama wa waathiriwa, maafisa wangu walikuwa na jukumu la kuhakikisha wataondoka kutoka eneo la kisa baada ya nyumba yote kubomolewa kabisa,” akaongeza.

Bw Kisang alitoa ilani kwamba wakazi waripoti visa vyote kwa idara za usalama kuhusiana na nyumba zinazoonyesha dalili ya kuwa dhaifu na kuhatarisha maisha ya watu kabla ya maafa kutokea wakati huu wa nsimu wa mvua ya masika.

Vilevile, aliagiza maafisa wake kuhakikisha watu wote wanaoishi karibu na mto Ngong wameondoka kabisa na kuhamia maeneo salama.

“Nimekuwa nikirudia kwamba serikali haitaki kupoteza maisha ya watu wake, kila uhai wa mtu ni muhimu. Watu waondoke karibu na mto na kuhamia katika vituo tulivyowatangazia hapo awali kuhamia hadi pale tutakapotoa mwelekeo zaidi,” akasema.