Habari Mseto

Familia 300 zilizoathirika kwenye mkasa wa moto Mukuru hazijapata nyumba rasmi miezi miwili baadaye

October 25th, 2020 2 min read

Na SAMMY KIMATU

ZAIDI ya familia 300 ambazo zilikosa makazi baada ya mkasa wa moto Mukuru, Kaunti ya Nairobi miezi miwili iliyopita hazijarudi makwao.

Wamiliki wa nyumba hizo hawajajenga nyumba mpya kutokana na changamoto za kiuchumi.

Akizungumza na Taifa Jumapili, mwenyekiti wa mtaa wa Mukuru-Hazina, Bw Mohammed Soba Kutuni amesema wamiliki nyumba zilizoteketea wanakabiliwa na shida za kifedha na kujenga nyumba zingine kutachukua muda mrefu.

Familia hizo zilipoteza nyumba zao wakati wa kisa cha moto mnamo Agosti mwaka huu. Mtaani huo huko maeneo ya South B, kaunti ndogo ya Starehe.

“Wamiliki wa nyumba wanasema hawana pesa za kujenga nyumba mpya baada ya kupata hasara kubwa ya mali ya thamani isiyojulikana siku hiyo. Wapangaji wamehifadhiwa na marafiki na jamaa zao katika mitaa mingine ya Mukuru. Isitoshe, wengine kadhaa waliondoka kwenda mashambani baada ya kupoteza kazi katika eneo la Viwanda baada ya kuripotiwa kwa janga la Corona,” Bw Soba amesema.

Vifusi vya mabaki ya zilizokuwa nyumba na bidhaa za kutumiwa nyumbani, vimeonekana katika eneo hilo na kuleta kumbukumbu za tukio baya.

Mhasiriwa na mama mfanyabiashara, Bi Juliana Kasyoka, 40, amesema alipoteza vitu vichache vya plastiki ambavyo alikuwa ameweka kwenye veranda yake.

Moto ulikatwa na na kuzuiwa na chumba chake kilichojengwa kwa mawe.

“Nilikuwa kazini kuja tu na kupata nguo, ndoo na mabeseni vyote vimeteketezwa lakini nyumba ilikuwa imara kwani ni yam awe na hivyo ikauzuia moto,” Bi Kasyoka, mama wa watoto wawili anakumbuka.

Mhasiriwa mwingine, Bi Rebecca Kemunto ambaye alikuwa na duka moja alisema mali yake yote ilibakia majivu. Mwanamke huyo aliyefadhaika alishtuka alipofika kwake na kuona iliyokuwa nyumba yake ilikuwa imeteketea yote.

“Vijana kutoka vitongoji vingine walipora mali wakijifanya ni Wasamaria wazuri,” anakumbuka.

Waathiriwa walitegemea chakula kilichopikwa na kilicholetwa kwa wiki moja na kusambazwa na wasamaria wema katika eneo hilo kulingana na Bw Soba.

Aliongeza kuwa mbunge wa eneo hilo, Bw Charles Njagua Kanyi alitoa misaada kwa waathiriwa ikiwa ni pamoja na mchele, blanketi na beseni.