Habari

Familia iachwe iomboleze kwa amani, Gideon asema baada ya Jonathan kufariki

April 20th, 2019 1 min read

Na CHARLES WASONGA

SENETA wa Baringo Gideon Moi ameomba kwamba familia ya Rais mstaafu Daniel Moi, iruhusiwe kuombeleza kifo cha kakake mkubwa, Jonathan Toroitich Moi, kivyao.

Jonathan Kipkemboi Arap Toroitich alifariki mnamo Ijumaa jioni, kulingana na taarifa ilivyotumwa Jumamosi na msemaji wa Mzee Moi Lee Njiru.

Kwenye taarifa, Gideon, ambaye ndiye kitinda mimba katika familia hiyo, alimtaja kakake kama mtu mpole, mwenye bidii na aliyependa kuishi maisha ya kawaida.

“Kama familia, tumekumbwa na huzuni kuu kufuatia kifo cha kakangu, Jonathan. Tunauliza mtuombee huku tukiomba turuhusiwe kuomboleza kivyetu,” akasema Seneta huyo. Hii ina maana kuwa huenda ni watu wachache tu wataruhusiwa kuhudhuria mazishi ya mwendazake.

Marehemu ambaye alikuwa mwendeshaji magari ya mashindano ya Safari Rally katika miaka themanini (1980s) amekuwa akiishi katika makazi yake yaliyoko eneobunge la Eldama Ravine.

Aliwania kiti cha ubunge katika eneo hilo mnamo 2013 lakini akashindwa na mbunge wa sasa Moses Lessonet.