Familia Kisumu yamtafuta mtoto aliyetoweka wiki tatu zilizopita

Familia Kisumu yamtafuta mtoto aliyetoweka wiki tatu zilizopita

Na BRENDA AWUOR

FAMILIA moja kutoka Manyatta, Kisumu, inaomba wanajamii kuisaidia kupata mtoto Brianna Atieno aliyepotea wiki tatu zilizopita.

Brianna, mtoto wa kike mwenye umri wa miaka mitano na mwanafunzi wa darasa la pili shule ya msingi Atlantic, Kisumu, alipotea nyumbani kwao mnamo Januari 26 mwendo wa saa kumi jioni alipoachwa na watoto wao wengine kumchunga.

Mtoto huyo alionekana mara ya mwisho akiwa amevaa rinda jeusi lenye mikono mifupi na viatu vya kijivu pamoja na shanga kwenye nywele.

Akiongea na ‘Taifa Leo’ kwa simu, babake Atieno, Bw Moses Ojango, amesema kuwa harakati za kumpata mtoto wake zimecheleweshwa kupitia wanaume watatu ambao wamekuwa wakimdanganya kuhusu aliko mwanawe.

”Nimekuwa nikidanganywa na wanaume watatu ambao nia yao ni kuniitisha pesa kabla ya kufichua aliko msichana wangu,” Bw Ojango alisema.

Alieleza kuwa amedanganywa na mtu kuwa afisa wa polisi ambaye aliwaambia wafike kituo cha polisi na Sh5,000 na kumpata mwana wao.

Baada ya kufika katika kituo cha polisi walioagizwa na kuulizia kwa jina waliloambiwa, walielezwa kuwa hamna yeyote katika kituo hicho mwenye jina hilo.

”Baada ya kufika katika kituo cha polisi tulichoagizwa, tulikosa kumpata aliyetuahidi na afisa wa kituo hicho kutuambia kuwa habari yoyote kuhusu mtoto haijafika katika kituo hicho,”alieleza.

Mtu wa pili kumdanganya Bw Ojango, ni dereva wa tuktuk aliyemwambia kuwa anamtambua dereva wa teksi aliyekuwa na mwanawe pamoja na wanawake wengine wawili walioshukishwa Bondo, Kaunti ya Siaya.

Kwa kuongea na dereva wa matatu kwa simu, aliitisha Sh7,000 kabla ya kufichua alipokuwa mwanawe.

Baada ya kutuma pesa mnamo Februari 2, 2020, dereva alikata mawasiliano baina yao.

”Nilituma pesa jinsi nilivyoagizwa Februari 2, 2020, lakini dereva aliamua kukatiza mawasiliano yetu,” alisema.

Wazazi wa Brianna kwa sasa wanaomba wanajamii wote pamoja na serikali kuwasidia kumpata baada ya kupiga ripoti katika kituo cha polisi Kondele pamoja na kituo cha polisi Kisumu Kati.

You can share this post!

Makundi ya kutetea haki yataka Bashir apelekwe Hague haraka

Kyle Walker atarajia mtoto na mwingine baada ya kutemwa

adminleo