Familia kortini kupinga hatua ya kuwahamisha

Familia kortini kupinga hatua ya kuwahamisha

Na MARY WAMBUI

FAMILIA zaidi ya 2,500 katika eneo la Mutomo, Gatundu Kusini, Kaunti ya Kiambu, zimepinga mpango wa kuwahamisha kupisha upanuzi wa Chuo Kikuu cha Mama Ngina.

Familia hizo zimeenda kortini huku zikisema kuwa hazikushauriwa kabla ya serikali kufikia uamuzi wa kuwataka kuhama kutoka kwenye ardhi ya jumla ya ekari 100.

Wameshtaki Tume ya Ardhi ya Kitaifa (NLC), Chuo Kikuu cha Mama Ngina, Chuo Kikuu cha Kenyatta na Wizara ya Elimu.

Kesi hiyo iliwasilishwa katika Mahakama ya Ardhi mjini Thika. Wanataka serikali ipigwe breki kutwaa ardhi hiyo wakisema kuwa wengi wa walalamishi ni wazee na wengine wamezika jamaa zao hapo.

“Familia nyingi zimezika wapendwa wao katika ardhi hiyo na itakuwa kinyume cha utamaduni na utu kufukua miili ya jamaa zao na kuihamishia kwingineko.

“Wengi wetu ni wazee wa kati ya umri wa miaka 60 na 100 na wanategemea jamaa zao kupata matibabu na riziki ya kila siku. Huwezi kuhamisha wazee kwenda kuanza maisha upya,” zinasema familia hizo.

Wakazi hao wanasema kuwa walipigwa na butwaa walipoona ardhi yao ikichapishwa katika Gazeti Rasmi la Serikali nambari CXXIII mnamo Septemba 27, mwaka jana.

Taarifa hiyo ya Gazeti Rasmi la Serikali iliwataka kuhama na kusalimisha mashamba yao kwa usimamizi wa Chuo Kikuu.

“Kulikuwa na orodha ya majina, nambari za ardhi na ukubwa wa eneo linalofaa kutwaliwa kwa lazima,” wanasema wakazi hao kupitia stakabadhi walizowasilisha mahakamani.

Mnamo Desemba 20, mwaka jana, NLC ilichapisha notisi nyingine kwa niaba ya Wizara ya Elimu ikiwataka wakazi 160 kuhudhuria mkutano wa kusikiliza malalamishi yao kuhusu fidia.

Mkutano huo utafanyika kati ya Jumanne, Januari 25, na Ijumaa, Januari 28, katika afisi ya chifu wa Mutomo.

“Mtu anayedai fidia ya ardhi yake, awasilishe malalamishi kwa njia ya maandishi na aambatanishe nakala ya kitambulisho cha kitaifa, nambari ya Mamlaka ya Ushuru (KRA), hatimiliki na namba ya akaunti ya benki,” ilisema notisi hiyo.

Familia hizo sasa zinataka shughuli hiyo kusitishwa ili kutoa nafasi kwa majadiliano zaidi.

“Walalamishi ndio wamiliki halali wa ardhi hiyo lakini hawajawahi kushauriwa na NLC au usimamizi wa Chuo Kikuu cha Mama Ngina,” wanasema.

Kesi hiyo iliwasilishwa mbele ya Jaji B.M Eboso mnamo Novemba, mwaka jana.

Jaji aliagiza pande zote zifike kortini Desemba 20 lakini baadaye majaji walienda likizo. Pande zote zinatarajiwa kukutana Januari 31, mwaka huu.

Mwanasheria Mkuu Kihara Kariuki, amepinga vikali ombi la familia hizo huku akisisitiza kuwa serikali ina uwezo wa kuchukua kipande cha ardhi kwa nguvu kwa mujibu wa Kifungu cha 40 (3) cha Katiba na Sheria ya Ardhi ya 2012.

Pia anasema kuwa masuala yanayolalamikiwa yangali yanajadiliwa hivyo ni mapema kukimbilia kortini.

Anasema masuala hayo yatapata ufumbuzi hivyo hakuna haja ya kwenda mahakamani.

  • Tags

You can share this post!

Gari lililojaa bangi lanaswa baada ya kuhusika kwenye ajali...

TUSIJE TUKASAHAU: Ripoti yasema kaunti zote 47 zinadaiwa...

T L