Habari

Familia kupewa mafunzo namna ya kuzika wanaofariki kutokana na Covid-19

August 11th, 2020 1 min read

Na SAMMY WAWERU

WIZARA ya Afya imesema itaanza kutoa mafunzo kwa familia za wanaofariki kutokana na maradhi ya Covid-19 ili wazikwe kwa utaratibu salama na unaofaa.

Shughuli hiyo pia itashirikisha baadhi ya wanakijiji, wizara ikisema hatua hiyo itasaidia kuondoa unyanyapaa katika jamii.

Waziri Msaidizi katika Wizara, Dkt Mercy Mwangangi amesema Jumanne mpango huo mbali na kuondoa unyanyapaa, unalenga kushirikisha wanafamilia katika kuwaaga wapendwa wao kama ilivyo desturi na itikadi za wengi katika hafla za mazishi.

Tangu maafa ya corona yaanze kushuhudiwa nchini, maafisa kutoka idara ya afya ndio wamekuwa wakizika walioangamizwa na virusi hivyo, wakiwa wamevalia vifaa maalum vya kujikinga (PPE) ili waepuke maambukizi.

“Suala la kuzika waliofariki kutokana na corona haswa kwa kuzingatia mavazi na vifaa tumekuwa tukilitia maanani sana. Wanaosaidia kuzika walioangamia lazima wawe na vifaa kamilifu (PPE) kuwazuia kuambukizwa virusi,” Dkt Mwangangi akaambia wanahabari, wakati akitoa takwimu za maambukizi ya Covid-19 nchini katika kipindi cha chini ya saa 24 zilizopita.

Kumekuwepo na visa vipya 497 vya Covid-19 hivyo kufikisha idadi jumla ya visa kuwa 27,425 tangu kisa cha kwanza Machi 13, 2020, nchini.

Akaeleza: “Tunapanga kuanza kuwapa mafunzo wanajamii katika kijiji cha wanaofariki, namna ya kuvalia PPE na jinsi ya kuzika wapendwa wao, ili tuondoe unyanyapaa kwa waathiriwa na katika jamii. Watu wa familia pia watahisi kuwaaga kwa njia ya heshima. Tunashughulikia suala hilo.”

Visa vya waliougua Covid-19 na kupona, pamoja na watu wa familia kutengwa katika jamii vinaendelea kuripotiwa.

Taswira hiyo pia si tofauti na ya waliofiwa, wanakijiji wakiepuka kutangamana nao kwa hofu ya kuambukizwa virusi.

Wizara ya Afya imekuwa ikihimiza umma kutobagua waliougua na kupona corona, pamoja na familia ya waathiriwa, ikisema yeyote anaweza kuambukizwa ugonjwa huo ambao sasa ni janga la kimataifa.

Kufikia Jumanne, Kenya ilikuwa imeandikisha jumla ya vifo 438 baada ya wagonjwa 15 kuthibitishwa kuangamizwa na Covid-19, katika kipindi cha saa 24 zilizopita.