Makala

Jinsi familia, mashabiki wa marehemu mwigizaji Pretty Mutave walivyomuenzi kipekee

September 27th, 2020 1 min read

Na MISHI GONGO

FAMILIA, mashabiki na marafiki wa marehemu mwigizaji Pretty Mutave walikusanyika katika ukumbi wa Swahilipot Hub mnamo Jumatano kumuenzi bingwa huyo wa telenovela aliyefariki Jumanne juma lililopita.

Bi Mutave alifariki alipokuwa anapelekwa hospitalini kwa matibabu.

Ilikuwa sherehe ya huzuni ambapo wote waliohudhuria walikuwa na maneno na sifa kedekede kwa mwendazake.

Wote waliyofika waliwasha mshumaa kwa heshima ya marehemu.

Marehemu Mutave alikuwa mwigizaji katika vipindi mbalimbali vya Kiswahili vikiwemo ‘Maza’, ‘Moyo’, ‘Aziza’ na vinginevyo.

Miongoni mwa watu waliofika katika sherehe hiyo ni meneja wa bodi ya udhibiti wa filamu eneo la Pwani Bw Bonventure Kioko ambaye alisisitiza ushirikiano kati ya waigizaji katika eneo la Pwani.

“Ni wakati wetu kushirikiana na kusaidia mmoja wetu anapokumbwa na tatizo,” akasema.

Mwigizaji Caro Rita katika hotuba yake alizungumzia jinsi sekta ya uigizaji ilivyoathirika kutokana na janga la corona.

Marehemu Mutave alizikwa jana Jumamosi nyumbani kwao Kibwezi, Kaunti ya Makueni.