Makala

Familia mbili Pwani zaitaka serikali izisaidie kupata jamaa waliochukuliwa na watu waliojitambulisha ni 'polisi'

November 2nd, 2020 2 min read

Na MISHI GONGO

FAMILIA mbili katika eneo la Pwani waomba msaada wa serikali kupata jamaa zao waliochukuliwa na watu wasiojulikana na ambao walijitambulisha kama maafisa wa polisi.

Familia ya Kondo kutoka eneo la Ramisi, Kaunti ya Kwale na ya Islam kutoka Majengo, Kaunti ya Mombasa walidai kuwa jamaa zao walichukuliwa na watu waliojitambulisha kama maafisa wa polisi lakini kufikia sasa hawajui walipo.

Walisema licha ya juhudi zao kuwatafuta hata katika mochwari, hospitali na vituo vya polisi katika eneo hilo hawajawapata.

Kulingana na Bi Mwanajuma Hassan mkazi wa Ramisi mwanawe Bw Haruni Kondo, 36, alitekwa nyara na watu wanne waliokuwa wamejihami kwa bunduki na kujitambulisha kuwa maafisa wa polisi mchama Alhamisi, Oktoba 29, 2020.

Mzazi huyo alieleza kuwa mwanawe ambaye ni mhudumu wa bodaboda alichukuliwa alipokuwa akisubiri abiria katika kituo cha Ramisi.

“Wenzake walioshuhudia walinieleza kuwa gari jeupe aina ya Probox nambari ya usajili KCD 432E lilifika katika maegesho ya bodaboda kisha kumchukua mwanangu baada ya kumtia pingu. Wenzake walipojaribu kudadisi watu hao walitoa bunduki na kusema kuwa ni maafisa wa usalama,” akasema Bi Hassan.

Alisema kabla ya kumteka nyara, gari hili lilionekana eneo hilo asubuhi.

“Gari hilo lilikuwa limeegeshwa nje ya nyumba yetu. Tulipowauliza iwapo walitaka kuvuka wakasema hapana na mwanangu alipotoka kwenda katika maegesho ya bodaboda walimfuata na kumkamata,” akasema Bi Hassan.

Kulia mwenye fulana ya bluu ni afisa katika shirika la Muhuri Francis Ouma, katikati ni Bi Mwanajuma Hassan mamake Haruni Kondo na kushoto ni Subira Kondo dadake Hassan Kondo. Picha/ Mishi Gongo

Kulingana na dadake Haruni, Bi Subira Kondo, kaka yake hajawahi kutuhumiwa na uhalifu wa aina yoyote.

“Ni mtu mwenye mke na mtoto wa umri wa miezi mitatu. Yeye ndiye tegemeo katika familia yetu hivyo tunaomba serikali itusaidie kuhakikisha kuwa mtoto wetu anarudi salama. Iwapo kuna kosa alilotekeleza basi tunaomba sheria za nchi zifuatwe kumhukumu,” akasema.

Mzazi mwingine Bi Rukiya Abdul Ali, alisema kuwa mwanawe mwenye umri wa miaka 17 alitoweka mwezi wa Septemba na hadi kufikia sasa hajui aliko.

Abdulsatar Islam alidaiwa kutoweka baada ya kumuaga mamake kuwa anaenda Mariakani.

“Mwanangu ni mshukiwa ambapo kwa mwaka mmoja sasa amekuwa akienda akiripoti kwa kituo cha polisi cha Urban kila mwanzo wa juma. Kabla kupotea alikuwa ameenda kupiga ripoti kisha siku ya pili akaniaga kuwa anaenda Mariakani kutembelea wakwe zake ambapo mpaka leo sijui aliko,” akasema Bi Ali.

Afisa wa shirika la kutetea haki za kibinadamu la Muhuri, Bw Francis Ouma, kuanzia mwezi Agosti hadi kufikia sasa watu watatu wamepotezwa katika eneo la Pwani.

Aidha alivitwika jukumu vitengo vya usalama kuwakamata wanaoshiriki katika kupotea na mauaji ya watu eneo la Pwani.

“Maafisa wa polisi wana jukumu la kuhakikisha usalama nchini hivyo iwapo wanakataa kuhusika na matukio hayo basi wanapaswa kuingilia kati kuhakikisha kuwa waliopotea wanaunganishwa na familia zao,” akasema.

Alisema wanaopotezwa mara nyingi huhusishwa na tuhuma za kuhusika na shughuli za kigaidi.

Alisema visa vya watu kupotezwa na wanaodaiwa kuwa maafisa wa polisi vimekithiri katika eneo la Pwani.

Alisema ndani ya miaka miwili, zaidi ya watu 100 katika eneo hilo wamepotezwa.

Septemba 2020, Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai aliwaonya Wakenya dhidi ya kuwahusisha maafisa wa polisi na visa vya utekaji nyara na mauaji yanayoendelea nchini.

Bw Mutyambai alisema visa hivyo vinatekelezwa na wahalifu wanaojifanya kuwa maafisa wa polisi.