Familia moja Gatuanyaga yaomba msaada baada ya jamaa wao kuuawa kinyama

Familia moja Gatuanyaga yaomba msaada baada ya jamaa wao kuuawa kinyama

Na LAWRENCE ONGARO

FAMILIA moja eneo la Gatuanyaga, Kaunti ya Kiambu, inataka usaidizi wa kifedha baada ya jamaa wao kuhifadhiwa chumba cha maiti kwa wiki moja huku wakikosa fedha za kuutoa mwili.

Simon Githae aliuawa kinyama ambapo mwili wake ulitolewa ngozi na sehemu nyingine muhimu.

Familia hiyo inasema wanahitaji kuchangisha zaidi ya Sh100,000 za kulipia ada ya kuhifadhi mwili huo kufanyiwa upasuaji na mipango ya mazishi.

Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika chumba cha maiti cha General Kago katika hospitali ya Thika Level 5.

Kulingana na familia hiyo, mwili huo ulipatikana ukiwa umetupwa kichakani bila nguo yoyote mwilini huku mwili ikiwa imeharibika kwa majeraha ya shambulio la kisu.

Mjane Bi Margaret Nyambura alisema mumewe alikuwa akifanya kibarua katika eneo hilo ambapo alipoondoka asubuhi, hakuweza kurejea nyumbani jioni.

Bi Nyambura ameiomba serikali ifanye juhudi kuona ya kwamba watu waliohusika wanakamatwa haraka iwezekanavyo.

“Mimi nimeachwa na watoto wawili na kwa hivyo kwa sasa sina uwezo wowote wa kuwalea,” alisema mjane huyo.

Familia ya marehemu inataka serikali kuingilia kati kwani marehemu ndiye alikuwa tegemeo.

Kunakosekana usalama eneo la Gatuanyaga na vitongoji vyake ambapo maafisa wa usalama wanastahili kupelekwa eneo hilo.

Wakazi wa eneo hilo wameachwa na hofu kubwa kwani kitendo walichomtendea marehemu ni cha kinyama.

Msemaji wa familia hiyo Bw Francis Njuguna alieleza kuwa marehemu alipatikaka uchi bila nguo mwilini na pia sehemu zake kadha zilikuwa zimekatwa.

“Tangu tukio hilo kutendeka wakazi wengi wameachwa na hofu huku ikiwalazimu kurejea nyumbani mapema majira ya saa 12 za jioni,” alisema Bw Njuguna.

Hata hivyo polisi wa eneo la Thika Mashariki wameanza uchunguzi huku maafisa wa upelelezi wakichukua usukani.

You can share this post!

Gareth Bale afunga bao lake la kwanza la La Liga tangu...

TAHARIRI: Heko chipukizi kuitawala dunia