Habari Mseto

Familia Mombasa yamtafuta mtoto aliyetoweka Jumamosi

July 15th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

FAMILIA moja eneo la Kisimani, Bombolulu katika eneobunge la Nyali inamtafuta mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka 13 aliyetoweka Jumamosi, Julai 11, 2020, katika hali isiyoeleweka.

Mtoto huyo kwa jina Dennis Kasala Amira alikuwa ametumwa kununua chakula sokoni Kongowea saa nne asubuhi, lakini kufikia saa nane mchana mama Angela Muthio Mutiso aliingiwa na wasiwasi kwa kukawia kwake.

Alichukua hatua ya kumtaarifu mumewe Abiud Amira aliyekuwa mjini Mombasa kwa shughuli za kikazi.

Bw Amira ameambia Taifa Leo kwamba mwanawe ni kijana mchangamfu na mwajibikaji na hivyo kutoweka kwake kumemsababishia hali ya mfadhaiko.

“Mke wangu aliponiambia mtoto ametoweka, nilirudi nyumbani na hadi kufikia usiku hakurejea na nikaamua kupiga ripoti katika kituo cha polisi,” amesema Bw Amira.

Aliripoti katika kituo cha polisi cha Nyali mnamo Jumapili ambapo afisa aliyekuwa katika zamu alimshauri kesho yake – Jumatatu – afike katika kitengo cha watoto.

Nambari ya tukio kituoni ni 39/12/7/2020 na maafisa wamemuambia kwamba watafanya uchunguzi na akipatikana watamwarifu.

Nambari ya simu ya baba wa mtoto huyo ni 0718292212 hivyo yeyote aliye na habari kumhusu anaweza kuwasiliana naye au kuripoti katika kituo chochote cha polisi.

Mtoto huyo ni wa darasa la saba.