Habari Mseto

Familia sasa yataka haki kwa mhadhiri aliyeuawa

February 29th, 2024 2 min read

STEVE OTIENO NA HILLARY KIMUYU

FAMILIA ya mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Nairobi aliyeuawa na mwili wake kupatikana ukiwa umetupwa katika kituo kikuu cha mabasi ya uchukuzi jijini Nairobi mnamo Februari 20, 2024 sasa inataka serikali iwachukulie hatua waliotenda uhalifu huo.

Akizungumza na Taifa Leo, kakake marehemu, Joseph Wambugu, alisema walikuwa wakiishi kwa wasiwasi kuhusu aliko Samuel Mararo tangu Februari 19, alipotoweka.

Hata hivyo, walipokea simu kutoka Kituo cha Polisi cha Kamukunji Jumanne, Februari 27 wakiombwa kuutazama mwili katika mochari ya City kuthibitisha ikiwa huo mwili ulikuwa wa mpendwa wao.

“Tulijawa na huzuni sana tulipoutambua mwili huo. Inavyoonekana, mwili wake ulikuwa umepatikana wiki moja iliyopita, Jumanne iliyopita na kupelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti mwendo wa saa 10 asubuhi,” Bw Wambugu alisema.

Walipokea simu hiyo takriban wiki moja baada ya wao kuripoti kisa hicho na walikuwa wamezuru hospitali kadhaa jijini humo kumtafuta marehemu Mararo.

Marehemu, mhadhiri wa muda katika Chuo Kikuu cha Nairobi tawi la Kisumu, alikuwa ameondoka nyumbani kwake Ijumaa jioni, Februari 16, kuhudhuria hafla ya mazishi Vihiga.

Aliondoka nyumbani kwake Kariobangi Kusini ambako aliwaacha watoto wake wawili wenye umri wa miaka mitatu na miezi tisa chini ya ulinzi wa mke wake. Alifika salama Vihiga na kuhudhuria mazishi Jumamosi.

Saa chache baadaye, aliabiri matatu hadi Kisumu ambako alikesha na kumfahamisha mkewe kuhusu mipango yake ya kuondoka Kisumu mwendo wa saa sita usiku, siku iliyofuata.

“Alimjulisha mkewe kwamba anasafiri Jumapili usiku wa manane na kwamba angefika nyumbani Jumatatu asubuhi. Hata hivyo basi hilo lilikuwa na hitilafu na kuchelewesha safari yao,” akasema Bw Wambugu.

Sasa, anaamini hiyo ndiyo ilikuwa mara yake ya mwisho kuzungumza na mumewe kwani baadaye alipokea simu za ajabu.

“Mkewe alianza kupokea simu za ajabu na ujumbe mfupi kutoka Jumatatu (Februari 19) kupitia WhatsApp. Mpiga simu aliendelea kuomba pesa kuanzia Sh500 hadi Sh1,000. Hapo ndipo alipojua kuwa huyo si mume wake na kumtaka huyo mtu ajitambulishe. Hapa ndipo nambari ya Samuel ilipozimwa hadi mwili wake ulipopatikana,” Bw Wambugu alisema.

Uchunguzi wa polisi ulibaini kuwa kufikia wakati simu ilipozimwa Jumatatu usiku huo, takriban Sh9,000 zilikuwa zimetolewa kutoka kwa M-pesa huko Kayole, Nairobi.

Uchunguzi zaidi pia ulibaini kuwa marehemu alifika Nairobi mwendo wa saa tisa jioni siku hiyo hiyo. Kwa sasa, familia yake inaomba serikali kuchunguza kisa hicho na wahusika wote wakamatwe.