NA RICHARD MUNGUTI
FAMILIA ya aliyekuwa dereva wa magari ya Safari Rally, Assad Khan imepinga vikali hatua ya polisi kufunga uchunguzi kabla ya uamuzi kutolewa ikiwa mpenziwe marehemu, Maxine Wahome atashtakiwa kwa mauaji au la.
Maxine alikuwa mpenziwe Assad na walikuwa wakiishi pamoja katika mtaa wa Kileleshwa, Nairobi. Wapenzi hao walikuwa madereza wa magari ya Safari Rally.
Kupitia wakili Danstan Omari, familia hiyo ya Assad ilisema inatazamia haki ifanyike ikitiliwa maanani mwanao alikufa katika mazingira tata.
Bw Omari alipinga vikali hatua ya polisi kufika kortini “kuomba faili ya kesi ifungwe ilhali hakuna aliyeshtakiwa”.
“Suala la kifo cha Assad Khan halipaswi kuchukuliwa vivi hivi. Familia ilipoteza mpendwa wao. Wanataka kujua hatua gani imechukuliwa dhidi ya mhusika katika kifo hicho,” Omari alimweleza hakimu mwandamizi Bernard Ochoi.
Wakili huyo aliteta kuwa polisi ndio waliomfikisha kortini Maxine kwa tuhuma alikuwa na habari muhimu ambazo zingewasaidia kutatua kitendawili cha kifo cha Assad.
Assad aliaga dunia mnamo Desemba 18, 2022 akipokea matibabu baada ya kupata majeraha akiwa katika makazi yake mtaani Kileleshwa, Nairobi siku kuu ya Jamhuri, Desemba 12,2022.
Walinzi katika makazi hayo ndio walimwarifu kaka yake mdogo wa Assad, Adil Khan aliyempeleka Nairobi Hospital na hatimaye akamhamisha na kumpeleka Hospitali ya Avenue alikofia.
Mawakili Steve Kimathi na Andrew Musangi waliomba mahakama ifunge faili hiyo ndipo mkurugenzi wa mashtaka ya umma (DPP) Noordin Haji atoe uamuzi ikiwa Maxine atashtakiwa kwa mauaji au la.
Hakimu mwandamizi Bernard Ochoi atatoa uamuzi Februari 15, 2023 ikiwa atatamatisha uchunguzi huo wa polisi au la ili DPP apate fursa ya kutoa agizo ikiwa Maxine atashtakiwa au la.
Polisi walimweleza hakimu wamepeleka faili ya kesi ya kifo cha Assad kwa DPP atoe mwelekeo.
Maxine alifikishwa kortini Desemba 13, 2022 na kuachiliwa kwa dhamana ya Sh100,000 hadi polisi watakapokamilisha uchunguzi kubaini ikiwa alihusika na kifo cha Assad.