Familia ya Cohen kutoa ushahidi zaidi

Familia ya Cohen kutoa ushahidi zaidi

NA RICHARD MUNGUTI

FAMILIA ya raia wa Uholanzi aliyeuawa na maiti yake kutupwa ndani ya shimo la choo imekubaliwa kuwasilisha ushahidi wa baruapepe aliyotuma marehemu Tob Cohen kwa dada yake Gabrielle van Straten inayoweza kufichua jinsi hali ilivyokuwa kabla ya kifo chake.

Katika barua hiyo Cohen alikuwa amemweleza dada yake kwamba “endapo atauawa na mkewe Sarah Wairimu Kamotho, amiliki mali yake.”

“Familia ya Cohen imekubaliwa kuwasilisha tena ushahidi kuhusu baruapepe anayodaiwa alituma marehemu kwa dada yake (Gabrielle),” Jaji Thande aliamuru.

Jaji Thande alitoa agizo ushahidi aliokuwa ameukataa urudishwe tena katika kesi ya kung’ang’ania mali ya Cohen kati ya familia yake na mkewe Sarah aliyeshtakiwa kumuua mumewe.

Jaji huyo alimkubalia wakili Philip Murgor anayemwakilisha mjane Sarah Wairimu Kamotho kujibu madai katika barua hiyo pepe.

“Kwa vile Gabrielle ameruhusiwa kuwasilisha barua hiyo pepe aliyotumiwa na Cohen, ninaomba korti iniruhusu niwasilishe ombi Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Jinai (DCI) George Kinoti kuwasilisha kortini Tarakilishi muundo wa Toshiba ya marehemu ikaguliwe kubaini ikiwa alimtumia dada yake barua hiyo pepe,” Bw Murgor alisema.

Pia mahakama ilimruhusu Murgor kuwasilisha ushahidi zaidi kuhusu barua hiyo pepe mnamo Agosti 29 kisha Bw Omari awasilishe ushahidi zaidi Septemba 13, 2022.

Kesi hiyo itatajwa Oktoba 19, 2022 kwa maagizo zaidi.

Na wakati huo huo Jaji Grace Nzioka anayesikiliza kesi ya mauaji dhidi ya Sarah Wairimu Kamotho alikataa kuisimamisha kusubiri uamuzi wa majaji watatu ikiwa alishtakiwa kwa njia halali.

Katika uamuzi wake, Jaji Nzioka alisema ombi hilo la Sarah halina mashiko kisheria kwa vile lilikuwa limesikizwa na kukataliwa na Jaji James Makau.

Jaji Makau alisema katika uamuzi wake kwamba “madai ya Sarah kwamba alishtakiwa pasipo na ushahidi wa kutosha yanaweza kuamuliwa na mahakama inayosikiza kesi ya mauaji inayo mkabili.”

Sarah anadai haki zake zilikandamizwa na Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Jinai (DCI) aliponasa mawasiliano ya simu ya Jaji Stellah Mutuku , wakili wake Philip Murgor na hata simu zake.

Anadai katika ombi hilo kwamba upande wa mashtaka ulikataa kumpa ushahidi wote ili aandae tetezi zake.

Anaomba majaji watatu wa mahakama kuu waamue ikiwa alishtakiwa kinyume cha sheria.

Pamoja na hayo Sarah anadai DCI na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) wamekuwa wakitoa taarifa kwa vyombo vya habari kwa lengo la kumfanya aonekane yuko na hatia ya kumuua mumewe kati ya Julai na Septemba 2019.

Bw Murgor aliomba akabidhiwe nakala ya uamuzi huo akate rufaa.

  • Tags

You can share this post!

Wajackoyah ampa Raila bonga points

Jaji Mkuu Martha Koome ateua majaji 3 kusikiliza kesi ya...

T L