Habari Mseto

Familia ya Gabriel Oguda yasema imempata akiwa hai


FAMILIA ya Bw Gabriel Oguda, afisa mkuu katika afisi ya Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kitaifa imetangaza kuwa amepatikana akiwa hai.

Bw Oguda alitekwa nyara kutoka nyumbani kwake Jumanne asubuhi na watu wasiojulikana ambao walimzuilia kwa zaidi ya saa 24.

Bw Zachary Oguda, nduguye ambaye amekuwa akimtafuta alisema kuwa aliwapata wale waliomteka nyara nduguye katika Mji wa Kajiado kabla yao kuingia haraka katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP).

“Nimewapata hawa watu mjini Kajiado na timu yao. Wameingia katika tawi la ODPP karibu na Bunge la Kaunti ya Kajiado na siondoki hapa bila ndugu yangu,” alisema Zachary.

Mapema jana, Bw Zachary aliwashutumu maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) kwa kumhamisha kaka yake kutoka kituo kimoja hadi kingine.

“DCI imekuwa ikituchezea siku nzima na sasa usiku umeingia. Wanaendelea kumhamisha kutoka kituo hadi kituo,” alisema.

Aliongeza kuwa kaka yake alikuwa hajala chochote tangu alipotekwa nyara.

Kutekwa nyara kwa Bw Oguda kulizua mjadala bungeni wabunge walipokuwa wakijadili Mswada wa Fedha.

Bw Wandayi alisema kuwa mwanaharakati huyo wa mitandao ya kijamii anayefanya kazi katika afisi yake alitekwa nyara kutoka kwa nyumba yake Jumanne saa mbili asubuhi na wanaume walioshukiwa kuwa maafisa wa polisi.

“Alisema kulikuwa na polisi kwenye lango lake walijaribu kuingia kwenye boma lake. Nilijaribu kupata mawakili kushughulikia hali hiyo lakini dakika 10 baadaye, simu yake ilizima,” kiongozi huyo wa wachache aliambia Bunge.

Wakati huo huo, Bw Oguda pia aliwasiliana na wafuasi wake kwenye mitandao ya kijamii akiwafahamisha kuhusu hali yake.

Masuala yaliyoibuliwa na Bw Wandayi yalimlazimu Spika Moses Wetang’ula kumwomba Inspekta Jenerali wa Polisi Japheth Koome awasiliane naye na kumfahamisha aliko Bw Oguda.

Taifa Dijitali imejaribu kuwasiliana na Msemaji wa Polisi Dkt Resila Onyango kuuliza ikiwa utekaji nyara wa hivi majuzi unaohusishwa na maandamano ya kupinga Mswada wa Fedha wa 2024 ulikuwa ukiendeshwa na polisi lakini hakujibu simu wala jumbe zetu.