Habari MsetoSiasa

Familia ya Ken Okoth yalia kutohusishwa kwa mipango ya mazishi

July 31st, 2019 1 min read

Na GEORGE ODIWUOR

FAMILIA ya baba ya aliyekuwa Mbunge wa Kibra, Ken Okoth inadai kwamba haijahusishwa katika mipango ya mazishi yake.

Familia hiyo inayotoka kijiji cha Kanyachir Amocho, eneo la Kochia katika eneobunge la Rangwe, Kaunti ya Homa Bay, ilisema haijashirikishwa katika maandalizi ya mazishi ya mbunge huyo.

Msemaji wa familia Raymond Mbai, jana alisema wangetaka mbunge huyo azikwe katika boma la marehemu baba yake eneo la Kochia.

Bw Mbai alisema hii itakuwa ni kuheshimu mila za jamii ya Waluo.

Hata hivyo, familia hiyo ilisema itaheshimu mapenzi ya mwendazake iwapo alitaka azikwe kwingineko.

Familia hiyo inasema wazazi wa Bw Okoth, Bw Nicholas Obonyo na Bi Angeline Ajwang walitengana mbunge huyo akiwa mchanga.

Kulingana na Bw Mbai, mbunge huyo aliondoka na mama yake wakarudi kijiji cha Ogenga, eneobunge la Kabondo Kasipul.

Kutengana huko kulimfanya Okoth kusahaulika katika boma la baba yake eneo la Kochia.

Msemaji wa familia alisema mbunge huyo ni mjukuu wa chifu mkuu aliyefahamika kama Obonyo aliyehudumu wakati wa ukoloni.

Baba ya mbunge huyo alikufa na kuzikwa Kochia 1993 katika ardhi ambayo babu yake alizikwa.

Aliomba familia kuheshimu wosia wa mbunge huyo iwapo alikuwa ameandika.