Habari za Kitaifa

Familia ya Kiptum kujengewa nyumba aushi kwa amri ya Ruto

February 16th, 2024 1 min read

NA MARY WANGARI

FAMILIA ya marehemu mwanariadha Kelvin Kiptum aliyeaga dunia mnamo Jumapili inatajengewa nyumba mpya ya vyumba vitatu vya malazi katika muda wa siku saba kabla ya mazishi yake.

Hii ni kufuatia agizo lililotolewa Rais William Ruto mnamo Ijumaa alipoamuru nyumba hiyo iwe tayari kabla ya Februari 24, 2024, tarehe iliyopangwa kwa ajili ya mazishi ya bingwa huyo mshikilizi wa rekodi ya mbio za marathon duniani.

Taifa Leo imebaini kuwa wajumbe maalum walizuru familia ya marehemu Kiptum kuwasilisha ujumbe kutoka kwa Kiongozi wa Taifa huku wakithibitisha kuwa Rais Ruto atahudhuria mazishi.

Mambo yote yako tayari huku timu ya wahandisi ikisubiri tu mawasiliano kutoka kwa familia ya Kiptum kuhusu itakapojengwa nyumba mpya.

Duru zinasema kuna maeneo matatu ambapo huenda akapumzishwa mwanariadha huyo aliyevunja rekodi ya mbio za masafa marefu ulimweguni.

Maeneo hayo ni ama boma la baba yake au katika kimojawapo kati ya vipande viwili vya ardhi alivyokuwa amenunua katika eneo la Kaptagat, Kaunti ya Uasin Gishu.

“Nataka kuwepo hapo, nataka kuwa ndani ya nyumba hiyo kabla ya Kiptum kupatiwa heshima yake ya mwisho kama shujaa jinsi alivyo,” alisema Rais Ruto.

Kiptum amemwacha mjane kwa jina Asenath Cheruto na kwa pamoja walikuwa wamejaliwa watoto wawili.

“Inamaanisha bingwa wetu tajika hakuwa na nyumba ya heshima kabisa au ni Rais aliyeamua kumjengea nyumba mpya kama zawadi ya kibinafsi kwa familia ya Kiptum?” akauliza mchuuzi mmoja jijini Nairobi aliyejitambulisha tu kwa jina Elvis.

Mwanariadha huyo aliyepangiwa kumenyana na nyota wa mbio hizo za masafa marefu Eliud Kipchoge alifariki papo hapo na mkufunzi wake raia wa Rwanda, Gervais Hakizimana.

Mwanamke aliyekuwa ndani ya gari pamoja na wawili hao alinusurika kifo.