Habari za Kitaifa

Familia ya marehemu Mark Too yapinga jaribio la maskwota

January 31st, 2024 2 min read

NA RICHARD MUNGUTI

FAMILIA ya aliyekuwa mwanasiasa mwenye ushawishi mwingi marehemu Mark Too pamoja na Mwanasheria Mkuu Justin Muturi wameomba Mahakama ya Upeo isiwaruhusu maskwota 10,000 kurudi katika shamba la ekari 25,000 lililo na thamani ya Sh3 bilioni katika Kaunti ya Uasin Gishu.

Lakini maskwota hao wamedai katika kesi waliyoshtaki mbele ya Jaji Mkuu (CJ) Martha Koome kwamba Mahakama hii ya upeo ilipotoka njia na mwongozo wa kisheria ilipowaamuru waondoke shambani.

Wanasema katika kesi itakayosikilizwa leo Jumatano kwamba mnamo Desemba 15, 2023, Koome, Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu, majaji Mohamed Ibrahim, Smokin Wanjala, Njoki Ndung’u, Isaack Lenaola, na William Ouko walitegemea ushahidi mpya kuamua kesi hiyo.

Kupitia kwa wakili William Arusei, maskwota hao wanasema ushahidi wa afisa wa ardhi Uasin Gishu R J Simiyu uliotegemewa kufikia uamuzi shamba hilo linamilikiwa na familia ya marehemu Too, haukuwa umewasilishwa katika Mahakama Kuu jaji Thomas Ombwayo alipoamua kesi hiyo.

Maskwota hao ambao mwenyekiti wao ni Bw Benjamin Ronoh, wamesema sheria inakataza ushahidi mpya kuwasilishwa katika mahakama wakati wa kusikilizwa kwa kesi ya rufaa.

“Sheria zinapinga ushahidi mpya kuingizwa katika kesi wakati wa kusikilizwa kwa rufaa. Ikiwa ushahidi huo mpya utakubaliwa, basi itakuwa ni kinyume cha sheria,” akasema Bw Rono katika ombi la maskwota kutaka Jaji Koome na wenzake wabatilishe uamuzi wa Desemba 15, 2023, na kuwaruhusu wamiliki shamba hilo walilopewa na hayati Daniel arap Moi.

Maskwota hao wameomba mahakama itumie mamlaka yake kubatilisha uamuzi wao kwa vile wamewasilisha ushahidi kuonyesha “ushahidi mpya ulipenyezwa kortini kinyume cha sheria na bila idhini ya mahakama.”

Bw Arusei amesema kuwa maamuzi ya hapo mbele ya mahakama hiyo katika uamuzi wa kesi ambao kiongozi wa Azimio Raila Odinga ilitupwa kwa vile aliwasilisha ushahidi kinyume cha sheria baada ya muda wa kuuweka kuyoyoma.

“Kampuni ya Fanikiwa Limited na familia ya Too na washtakiwa wengine waliwasilisha ushahidi mpya uliotegemewa kuamua mzozo wa umiliki wa shamaba hili. Uamuzi huu unafaa kutupiliwa mbali na maskwota kuruhusiwa kumiliki shamba hilo la ekari 25,000,” asema Bw Arusei.

Maskwota hao pia wanasema walipewa shamba hilo na Kamishna was Ardhi baada ya kuidhinishwa na hayati Moi.

Lakini Mwanasheria Mkuu na familia ya Too wamepinga ombi la maskwota uamuzi huo ubatilishwe wakidai ni mbinu ya kufungua upya kesi hiyo na ilikuwa imekamilishwa.

Wakili Fred Ngatia anayewakilisha familia ya Too amesema kuwa sheria haziruhusu Mahakama ya Upeo kufungua kesi kama imekamilika kusikilizwa na uamuzi kutolewa.

Bw Ngatia ameomba kesi ya maskwota hao wanaotambulika kwa jina Sirikwa Squatters Group (SSG) isikubaliwe.

Familia hiyo na Muturi (AG) wanasema kesi ikikamilika huwa imekamilika na kamwe haiwezi kufunguliwa.

Wanadai maskwota hao wanadai Moi aliruhusu wapewe shamba ilhali hawakumuita alipokuwa hai kuthibitisha madai hayo.

Lakini Bw Arusei amewajibu akisema Kamisha wa Ardhi na Moi waliwapa maskwota shamba hilo na suala la umiliki wao sio la kujadiliwa tena.

Bw Arusei pia ameomba ushahidi wa Kamishna wa Ardhi na maafisa wengine watano utupiliwe mbali akisema uliwasilishwa siku nyingi baada ya muda uliotengwa na Mahakama ya Upeo mnamo Desemba 20, 2023, kupita.

Kesi hiyo itatajwa Januari 31, 2024, kwa maagizo zaidi.