Habari Mseto

Familia ya mwanahabari aliyeuawa yafika kortini ifidiwe

March 3rd, 2020 1 min read

Na Joseph Openda

FAMILIA ya mwanahabari aliyeuawa miaka 17 iliyopita, William Munuhe, imewasilisha kesi mahakamani kuilazimisha serikali iisaidie kupata haki.

Familia hiyo kupitia nduguye marehemu Muhuhe, Josephat Muriithi Gichuhi, iliwasilisha kesi hiyo katika Mahakama ya Nakuru huku ikiikashifu serikali kwa kile ilichotaja kama kuvuruga uchunguzi na hivyo kuwanyima haki.

Bw Munuhe alipatikana amefariki katika nyumba yake ya kupanga mnamo Januari 17, 2003. Kifo chake kilihusishwa na kazi yake ya uchunguzi ambayo ililenga kusaidia kukamatwa kwa mshukiwa wa mauaji ya halaiki nchini Rwanda, Felicien Kabuga.

Kabuga amelaumiwa na jamii ya kimataifa kuhusiana na mauaji hayo ya takriban watu milioni moja kwa kipindi cha siku 100.

Familia hiyo inataka serikali ilazimishwe kuilipa ridhaa na itangaze ikiwa mtoro huyo (Kabuga) yuko hai au amefariki. Kwenye stakabadhi alizowasilisha mahakamani, Bw Mureithi anadai serikali imefeli kuendesha uchunguzi kubaini ukweli kuhusu kifo cha nduguye.

meikosoa serikali kwa kufeli kuendesha uchukuzi wa umma ambao ungesaidia kukamatwa kwa wale waliohusika na kifo cha Bw Munuhe.

Kulingana na Bw Mureithi serikali inajivuta kufuatilia kisa hicho ilhali ilifeli kutoa ulinzi wa nduguye ambaye anadai aliuawa kutokana na kazi yake kama mwanahabari mpekuzi.