Habari Mseto

Familia ya polisi 'aliyejiua' yadai haki

July 30th, 2018 1 min read

Na SAMMY LUTTA

FAMILIA ya afisa wa polisi aliyedaiwa kujinyonga katika Kaunti ya Isiolo sasa inataka kupata haki baada ya mwili kupatikana na majeraha ya risasi. Konstebo Kelvin Aleper Nyanga, 23, wa Kikosi cha Kukabiliana na Dharura (RDU) alikuwa akifanya kazi katika kambi ya Ngarmara hadi mauti yake Julai 11.

Bi Marcella Karenga, dada ya mwendazake alisema maafisa wa RDU wa Isiolo walidai kuwa Aleper alijitia kitanzi lakini familia imepuuzilia mbali taarifa hiyo.

“Tunashuku kwamba jamaa yetu aliuawa kwa risasi. Tunaomba Tume ya Kitaifa ya Haki za (KNCHR) kuanzisha uchunguzi ili kubaini ukweli kuhusu kilichosababisha kifo cha ndugu yangu,” akasema.

Familia ilishikilia kuwa jamaa yao hakuwa na jambo lolote lililokuwa likimsumbua hadi kufikia hatua ya kujiua.

“Tunaamini kuwa aliuawa na tuna haki ya kujua ukweli,” akasema Bi Karenga.

“Nilipigia simu na Inspekta Hassan kutoka Isiolo aliyenifahamisha kwamba ndugu yangu alijiua. Nilimuuliza ikiwa kweli walishuhudia akijiua, wakanijibu kwamba walipata mwili wake bila kujua kiini cha mauti yake.

“Juzi Inspekta alinieleza kwamba ndugu yangu alienda hospitalini kupimwa na aliporejea alikuwa na huzuni. Madai hayo yote hayana mashiko,” akaongezea.

Familia yake inasema kuwa maafisa wenzake walitelekeza mazishi ya mwendazake, kama ishara ya kuonyesha kuwa alijitoa uhai. Waziri wa Kilimo wa Turkana Chris Aletia ambaye pia ni jamaa ya mwndazake alisema hata maafisa walioleta maiti ya mwendazake nyumbani hawakuvalia sare za polisi.

Viongozi wa Turkana wakiongozwa na kiongozi wa Chama cha Thirdway Alliance Party Ekuru Aukot na mbunge wa Loima Jeremiah Lomorukai walihusisha kifo cha Aleper na operesheni dhidi ya wezi wa mifugo inayoendelea katika Kaunti ya Isiolo.

Wanasiasa hao walidai kuwa huenda aliuawa baada ya kushukiwa kuwa huenda alifichua siri kuhusu wizi wa mifugo kwa watu wa jamii yake ya Waturkana.