Habari Mseto

Familia ya Rai tayari kununua Aquamist

May 5th, 2019 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

Familia ya Rai, inayomiliki kampuni ya maji ya Menengai, inalenga kununua kampuni ya utengenezaji wa vinywaji ya Aquamist.

Mamlaka ya Ushindani(CAK) imetoa idhini kwa pendekezo hilo la kutwaa hisa zote za Aquamist, inayomilikiwa na Aquapani Limited.

“Kutokana na kuwa ununuzi huo huenda usisababishe ushindani mbaya au hofu kwa umma, Mamlaka hii imeidhinisha ununuzi kwa asilimia 100 ya hisa zilizotolewa kwa Aquamist na Aquapani Limited,” CAK ilisema katika taarifa.

Hatua hiyo itaiwezesha Menengai kuimarika katika utengenezaji wa vinywaji visivyo pombe. Zaidi ya kupakia maji na kuyasambaza, Aquamist pia hutengeneza sharubati aina ya Vita na chai ya barafu pamoja na maji yaliyotiwa rangi. Kampuni hiyo huwa inauza bidhaa zake kwa mahoteli na mikahawa mikubwa.

Kampuni hiyo ambayo inamilikiwa na familia ya Premji ina soko la asilimia tisa Nairobi na asilimia nne kitaifa. Mshindani wake, Maisha drinking water, ambayo inasimamiwa na Ketepa ina soko la asilimia nane.

Maji ya Dasani, yanayotengenezwa na kampuni ya Coca Cola ndiyo yanayoongoza nchini kwa asilimia 23, kulingana na takwimu za Euromonitor.

Familia ya Rai pia inashiriki utengenezaji wa bidhaa za jikoni kama vile sabuni, mafuta na vile vile bidhaa za mbao.

Baadhi ya bidhaa ambazo hutengenezwa chini ya familia hiyo ni Top Fry, Somo Fry na Karibu.