Habari

Familia ya Raila, mjane wa Fidel wapewa wiki mbili kusuluhisha mgogoro nje ya mahakama

November 13th, 2019 1 min read

Na SAM KIPLAGAT

MAHAKAMA imewapa Ida Odinga na Lwam Bekele ambaye ni mjane wa marehemu mwanawe Fidel Odinga, hadi Novemba 27, 2019, wawe wamesuluhisha mzozo wa mali ya marehemu nje ya korti huku pia ikimuongeza mama ya watoto pacha wanaodaiwa kuwa ni damu ya kifungua mimba wa kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Pande zote zimefika Jumatano mbele ya Jaji Aggrey Muchelule, ambapo zimesema zimekuwa zikifanya mashauriano kusuluhisha kesi nje ya mahakama.

Familia ya Bw Odingas imemshtaki Lwam ikimlaumu kwa kile imetaja ni kuwatenga watoto pacha ambao mama yao mzazi ni Phoebe Akinyi Gweno.

Ida na bintiye Winnie Odinga, katika wasilisho lao wanasema Lwam anafahamu uwepo wa pacha hao lakini kimaksudi ameamua “kuwapiga kikumbo nje ya urithi wa mali.”

Oktoba 2019 Jaji Muchelule aliagiza uchunguzi wa vinasaba (DNA) kubainisha ni nani baba mzazi wa watoto pacha wa Gweno, ingawa haujafanyika.

Bi Gweno katika wasilisho lake anataka ahusishwe katika kesi hiyo ili kuyaweka mambo bayana kuhusu wanawe.

“Mteja wangu anataka kuyaweka mambo sawa,” wakili wake Bw John Swaka alisema.

Kesi itatajwa Novemba 27, 2019.