Habari Mseto

Familia ya Sharon yakejeli wanaodai mazishi yatagharimu Sh2.7 milioni

October 15th, 2018 1 min read

Na MWANDISHI WETU

KAMATI inayoandaa mazishi ya Bi Sharon Otieno, ambaye alikuwa mpenzi wa Gavana wa Migori, Bw Okoth Obado, imewalaumu watumizi wa mitandao ya kijamii kwa kutatiza mipango yake.

Kamati hiyo ilisema watumizi wa mitandao ya kijamii wanaharibia familia hiyo sifa kwa kueneza uwongo kuhusu mipango ya familia.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Bw Elijah Opiyo, alitaja baadhi ya uvumi unaoenezwa kwenye mitandao ya kijamii kama madai kuwa wamepanga kutumia kiasi kikubwa cha fedha katika mazishi hayo.

Kumekuwa na madai yanayoenezwa mitandaoni kwamba bajeti ya kumzika mwanafunzi huyo wa Chuo Kikuu cha Rongo ni Sh2.7 milioni.

Bw Opiyo alisema madai hayo yameathiri juhudi za familia ya marehemu kutafuta usaidizi wa kifedha kutoka kwa wasamaria wema.

Alifafanua kuwa familia hiyo ina bajeti ya Sh1.2 milioni.

Bi Otieno aliuawa Septemba, na Gavana Obado ameshtakiwa kwa mauaji yake kwenye baadhi ya mitandao ya kijamii.

Mitandao inayoeneza madai hayo ilidai tarehe ya mazishi ilibadilishwa ili isifanyike siku moja na ile ya aliyekuwa mwenyekiti wa baraza la mji Nyanza Kusini, Bw Aketch Chieng’ ambaye amepangiwa kuzikwa Oktoba 19. Mazishi hayo mawili yatakuwa katika kaunti moja ya Homa Bay.

“Kuna watu wanadhani tumebadilisha mipango yetu kwa sababu waomolezaji watatatizika kuhudhuria mazishi mawili kwa siku moja. Mipango yetu haitaingilia kivyovyote mipango inayoendelea katika boma la marehemu Chieng’,” akasema.