Habari

Familia ya waliozama katika kivuko cha Likoni sasa yalalama miili kucheleweshwa

October 15th, 2019 2 min read

Na MISHI GONGO

FAMILIA ya mwanamke na mwanawe waliozama katika kivuko cha Likoni Septemba 29, 2019, sasa inalalamika ikisema inacheleweshwa kukabidhiwa miili ili ikaizike.

Maiti za marehemu Mariam Kighenda aliyekuwa na umri wa miaka 35 na mwanawe Amanda Mutheu ziliopolewa Ijumaa wiki jana baada ya miili yao kukaa ndani ya bahari kwa muda wa siku 13.

Mumewe marehemu – Bw John Wambua – sasa anadai maafisa wa usalama wamedinda kuachilia miili hiyo kwa mazishi licha ya miili hiyo kuwa katika hali mbaya.

Akizungumza na Taifa Leo kwa simu Bw Wambua amesema walikuwa wamepanga kusafirisha miili ya wawili hao hadi Kilomeni, Kaunti ya Makueni kwa mazishi mnamo Jumatatu.

“Tulikuwa tumepanga kuwazika Jumatatu lakini kwa sababu maafisa wa polisi wamedinda kuachilia miili hiyo, imebidi tusogeze mbele tena siku ya mazishi,” amesema Wambua.

Aidha amesema hakuna taarifa yoyote waliopewa kuhusiana na kucheleweshwa kukabidhiwa miili ya wapendwa wao.

“Tulielezwa kuwa upasuaji wa miili kwa ajili ya uchunguzi ungefanyika Jumatatu lakini haukufanyika na hadi kufikia sasa hatujaelezwa ni kwa nini shughuli hiyo haikuendelea,” akasema.

Bi Kighenda na mwanawe walizama katika kivuko cha Likoni Feri Septemba 29 baada ya gari lao aina ya Toyota ISIS kutoka ndani ya feri na kutumbukia baharini.

Kamanda wa polisi katika eneo la Likoni mjini Mombasa Bw Benjamin Rotich alisema upasuaji huo ulitarajiwa kufanyika katika hospitali kuu ya Pwani; Makadara lakini tena ikaelezwa mamlaka ya hospitali hiyo haijafanya upasuaji huo.

“Uchunguzi wa miili hiyo ulipangiwa kufanyika katika hospitali ya Makadara lakini kufuatia sababu wanazozijua wenyewe hawajafanya hivyo na tukalazimika kutafuta sehemu nyingine,” akasema Kamanda huyo.

Ameongezea kuwa hawengeweza kuachilia miili hiyo kwa familia kwa shughuli za mazishi ikizingatiwa kesi ilifunguliwa uchunguzi wa chanzo cha vifo vya wawili hao ukihitajika ambapo ripoti ya upasuaji wa maiti inahitajika.

“Lazima tunakili majibu ya uchunguzi wa upasuaji wa miili hiyo ili kuendeleza uchunguzi,” akaeleza.

Bw Rotich amesema upasuaji huo unatarajiwa kufanyika Jumatano katika hospitali binafsi ya Jocham ambapo miili ya wawili hao imehifadhiwa tangu kuopolewa kwao kutoka baharini.