Habari Mseto

Familia ya Waluke yaomba Wakenya wamchangie faini

June 29th, 2020 1 min read

Na MWANDISHI WETU

FAMILIA ya Mbunge wa Sirisia, John Waluke sasa inaomba msaada kutoka kwa umma ili kulipa faini itakayomwezesha kuachiliwa huru.

Bw Waluke alihukumiwa kifungo cha miaka saba gerezani wiki iliyopita, au alipe faini ya Sh727 milioni baada ya kupatikana na hatia ya kulaghai Bodi ya Kitaifa ya Mazao na Nafaka (NCPB) Sh297 milioni.

Alihukumiwa pamoja na Bi Grace Wakhungu ambaye ni mkurugenzi mwenzake wa kampuni ya Erad iliyohusika katika ulaghai huo.

Jumapili, mkewe mbunge huyo, Bi Roselyne Waluke alitoa wito kwa umma kutoa mchango wa kifedha ili kumwokoa mumewe.

“Kama mnavyojua, shida imetupata na tunashukuru wote ambao wamesimama nasi kwa maombi. Ninaomba kwamba muendelee kuwa pamoja nasi. Mtuombee na ninaomba msaada wa kifedha kutoka kwenu wakati huu; tuchange kwa ukarimu na Mungu atawabariki,” akasema, kupitia kwa kanda ya sauti iliyosambazwa mitandaoni.

Washtakiwa hao wawili walihukumiwa na Hakimu Mkuu Elizabeth Juma, hukumu ambayo imesifiwa na wengi kuwa funzo kwa wanaojihusisha katika uporaji wa mali ya umma.