Habari za Kitaifa

Familia yaeleza jinsi binti yao wa miaka 20 aliuawa kikatili Roysambu

January 17th, 2024 1 min read

NA WANDERI KAMAU

HATIMAYE, familia ya msichana aliyeuawa kikatili kwenye nyumba moja ya malazi katika eneo la Roysambu, Kaunti ya Nairobi, usiku wa kuamkia Jumapili, imejitokeza na kueleza jinsi mwana wao alikumbana na mauti yake.

Msichana huyo ametambuliwa kama Rita Waeni Muendo, 20,  ambapo alikuwa akielekea mwaka wa nne katika Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta (JKUAT).

Kwenye taarifa Jumatano, familia hiyo ilisema kuwa mwanao aliondoka nyumbani kwa shangaziye Jumamosi, Januari 13, 2024 katika eneo la Syokimau, Kaunti ya Machakos, ili kukutana na rafiki.

Mnamo Jumapili, Januari 14, babake alipokea ujumbe kutoka kwa simu ya msichana huyo, ukimtaka kutuma fidia ya Sh500,000 kwa muda wa saa 24 ili aachiliwe huru.

“Kutokana na ujumbe huo, tuliripoti tukio hilo kwa polisi na Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI). Tulitumiwa jumbe mbili zaidi zikituagiza kulipa fidia,” ikaeleza familia hiyo.

Familia hiyo, hata hivyo, haikufanikiwa kupata maelezo zaidi kuhusu fidia hiyo au njia ya kujadiliana na watu hao kuhusu ulipaji wa fedha hizo.

“Tulipewa masharti zaidi wakati mtoto wetu alikuwa ashauawa,” ikaeleza.

“Baada ya kumtafuta mtoto wetu kwa uchungu mwingi kwa ushirikiano na DCI, tulimtambua kama msichana aliyeuawa kikatili usiku wa kuamkia Jumapili karibu na duka la jumla la Thika Road Mall (TRM),  Januari 14. Tunaamini alihadaiwa na muuaji wake, aliyejaribu kutwitisha pesa, hata baada ya kumuua,” ikaeleza.

Ikaongeza: “Tuna masikitiko mengi kutokana na kifo cha Waeni, hasa jinsi alivyouawa. Tunatatizika kukubali uhalisia wa tukio hili.”

Familia hiyo ilimtaja binti yao kuwa mwerevu kuzidi umri wake, mjalifu, mkarimu na aliyekuwa mchangamfu daima.

Mnamo Jumanne, polisi walisema kuwa washawakamata washukiwa watatu kutokana na mauaji hayo.

Kulingana na polisi, mmoja wa washukiwa hao ni raia wa Nigeria, aliyenaswa akijaribu kusafiri nchini humo katika Uwanja wa Kitaifa wa Ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA).