Familia yahangaika baada ya kupata mwili uliokuwa umetoweka kaburini

Familia yahangaika baada ya kupata mwili uliokuwa umetoweka kaburini

Na MAUREEN ONGALA

FAMILIA ya marehemu Fatuma Mwero kutoka kijiji cha Mabirikani, Kaunti ya Kilifi ambaye mwili wake ulikuwa umetoweka katika kaburi lake wiki iliyopita, wamelalamika kuhangaishwa kufanya mazishi upya baada ya mwili huo kupatikana wikendi.

Marehemu aliyefariki akiwa na umri wa miaka 77 alikuwa amezikwa Februari 27, lakini kaburi lake likapatikana liko wazi wiki iliyopita.

Mwili wake ulipatikana takriban mita 600 kutoka kwa kaburi hilo Jumapili.

Wamelalamika kuwa walishindwa kuuzika tena baada ya polisi kudai kwamba kuna agizo la mahakama kuwazuia kufanya mazishi katika ardhi hiyo ya ekari 15 iliyo Kaunti Ndogo ya Rabai.

Hii ni baada ya Kamanda wa polisi wa Kaunti Ndogo ya Rabai, Bw Fredrick Abuga kusema familia hiyo ilipewa amri ya mahakama kuwazuia kufanya mazishi hapo.

Familia hiyo inasisitiza hawakupewa amri ya mahakama na wanasema sehemu hiyo ya ardhi ni ya makaburi ya familia yao.

Msemaji wao, Bw Dickson Kenga, alisema wanahangaika sana kwa vile mwili umerudishwa kuhifadhiwa katika mochari ya Hospitali Kuu ya Pwani mjini Mombasa ilhali walikuwa wamekamilisha mazishi.

“Mwili wa mama yetu ambao ulikuwa umeibiwa ulirudishwa baadaye ukatupwa mbali kutoka kaburini. Tulitaka kuuzika siku hiyo hiyo lakini polisi wakasisitiza kuna agizo la mahakama kwa hivyo tuupeleke mochari na tutafute sehemu nyingine ya kuzika mwili huo,” akasema.

Alisema mwili huo bado uko ndani ya jeneza na wanahofia utaanza kuoza.

Mwili mzima wa Bi Mwero ulionekana na watoto waliokuwa wamepeleka mbuzi malishoni mwendo wa saa saba mchana Jumapili.

“Hatutamzika mahali popote kwingine kwa sababu hatukuwa tumemzika kwa ardhi ya mtu yeyote bali ni ardhi yetu,” akasema.

Kabla Jumapili, familia hiyo ilikuwa imekata tamaa kuupata mwili huo wakaamua kufanya ibada maalumu na kufunika kaburi lake wakiongozwa na Mzee Juma Lwambi ambaye ni mumewe marehemu.

Familia hiyo inashuku mwekezaji anayedai kumiliki ardhi hiyo ndiye alihusika katika ufukuaji wa mwili wa marehemu, lakini polisi wamesema uchunguzi bado unaendelea kubainisha ni nani aliyehusika.

You can share this post!

Hadhi: Wito serikali iimarishe majukwaa ya kazi za sanaa...

Njia asili ya kuondoa visunzua yaani warts