Habari Mseto

Familia yakataa kuzika jamaa asiye na kichwa

September 10th, 2019 1 min read

DENNIS LUBANGA na SUSAN TOWETT

MAZISHI ya mwanaume mwenye umri wa miaka 42 kutoka kijiji cha Lukhokhwe, Kaunti ya Bungoma aliyepoteza maisha baada ya kuhusika kwenye ajali ya barabarani nchini Malawi huenda yasifanyike hivi karibuni baada ya mwili wake kurejeshwa nchini bila kichwa chake.

Familia ya marehemu Geoffrey Wekesa Jumanne iliapa kutozika mwili wa mwendazake hadi pale kichwa chake kitakapopatikana.

“Ni mwiko katika tamaduni na mila za jamii ya Wabukusu mwili kuzikwa bila kichwa kwani hatua hiyo inaweza kutuletea laana,” alisema Mzee Binom Khaemba, babake marehemu.

Hadi wakati wa kifo chake, Wekesa alihudumu kama dereva katika kampuni ya kutengeneza mapipa ya maji ya Exo Tank iliyo na makao yake eneo la Athi River.

Alifariki nje ya jiji kuu la Malawi la Blantyre baada ya lori alilokuwa akiendesha kupata ajali na kubingiria mara kadhaa.

Ajali hiyo ilitokea Agosti 21, siku tatu baada ya mwendazake kufika nchini humo kutoka Mombasa.

Mwili wake ulirejeshwa nchini wiki iliyopita na unahifadhiwa katika chumba cha maiti cha Kiminini lakini familia imedinda kuchukua mwili huo kwa mazishi.

Bi Susan Nasimiyu ambaye ni mke wa marehemu ameomba serikali kupitia wizara ya mambo ya nje kusaidia kufanya upelelezi kuhusu kifo cha mumewe.

“Naomba serikali inisaidie kwa sababu siwezi pekee yangu. Ingekuwa vyema ikiwa serikali ingenipeleka katika eneo la tukio la ajali ili niweze kuona kama nitapata kichwa hicho,” alisema Bi Simiyu.

Bw Alex Wekesa ambaye ni jirani yake mareheru alielezea kuwa marehemu alikuwa ni tegemeo kwenye familia yake na alikuwa akipania kununulia jamaa wake kipande cha shamba.

“Familia hii haijiwezi kwani hawana mahali pa kuishi. Ilikuwa ni hamu ya marehemu kutafuta riziki na hela ili akanunue kipande cha shamba cha kusitiri familia yake,” alisema Bw Makhanu.

Familia hiyo imeapa kuwa haitatoa mwili wa marehemu katika chumba cha kuhifadhi maiti hadi kichwa chake kitakapopatikana.