Makala

Familia yamlilia Uhuru aingilie kati Tanzania imwachilie huru mwanao

December 31st, 2018 2 min read

Na SAMUEL BAYA

Familia ya kijana wa umri wa miaka 28 ambaye alipotea wiki iliyopita katika mpaka wa Kenya na Tanzania sasa inamtaka Rais Uhuru Kenyatta na mwenzake wa Tanzania John Magufuli kuingila kati na kumtoa kijana wao.

Khamis Zuma kutoka eneo la Kinango aliondoka nyumbani kwao Desemba 5 na kuaga familia akiwemo mkewe kwamba alikuwa akielekea Tanzania kutafuta ajira.

Na hapo jana, familia hiyo ikiongzwa na baba yake mzazi Mohamed Ngome, 41 na mkewe Zaituni Abeid, 27 waliwahutubia waandishi wa habari katika afisi za shirika la kutetea haki za kibinadamu la Haki Africa wakiomba mtoto wao apatikane.

Waliandamana katika kikao hicho cha wanahabari na mkurugenzi mkuu wa shirika hilo Bw Khalid Hussein pamoja na maafisa wengine.

“Tangu mwanangu apotee wiki iliyopita, mimi sijapata usingizi wowote. Niko na maradhi ya presha na kwa sasa hali yangu si nzuri. Ninachoomba mimi ni kumtaka mwanangu apatikane tu arudi nyumbani,” akasema Mzee Ngome.

Kulingana na baba yake, kijana huyo aliondoka na kuvuka upande wa Kenya na kisha baadaye akaingia ndani ya Tanzania na hapo ndipo ambapo alikamatwa.

“Mwanangu alijaribu kunipigia simu mara kadhaa lakini ilipofika jumatatu jioni, alinitumia ujumbe kupitia kwa simu yake kwamba amepita vizuri katika upande wa Kenya lakini amekamatwa na anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Duga kilichoko katika upande wa Tanzania.

Kituo hicho kiko tu mwendo wa dakika tano tu kutoka mpaka wa mataifa hayo mawili,” akasema mzee huyo.

Mzee huyo alisema kuwa kwa vile ilikuwa usiku alisubiri mpaka asubuhi ndipo akaelekea katika kituo hicho cha polisi lakini majibu ambayo aliyapata yalimvnjua moyo.

Aidha Mzee Ngome alisema polisi katika kituo cha Duga polisi hao wa Tanzania walimwambia kwamba hawakuwa na habari zozote na hivyo basi wakamtaka arudi katika kituo cha polisi cha Horohoro.

“Katika kituo cha polisi cha Horo Horo afisa mmoja wa polisi baada ya kusikiliza kilio changu aliniunganisha na afisa mmoja katika afisi ya uhamiaji ambapo nilikutana na afisa mwengine,” akasema Mzee Ngome.

Katika afisi hiyo ya uhamiaji Mzee Ngome alisema kuwa afisa mmoja alimueleza kwamba kijana huyo alimuona akikamatwa lakini hakujua ni nani ambaye alikuwa akimshika, lengo na madhumini.

“Baada ya maelezo hayo nilijua kwamba afisa huyo atanisaidia ila muda mchache aligeuka na kusema hana habari zaidi ya hayo na jambo la muhimu ilikuwa ni kumtafuta mwanangu na kumuuliza ni kwani alikamatwa,” akasema.

Tukio la kupotea kwa mwanawe alisema limetatiza kabisa mipango ya familia na linamtesa vibaya mamake.

“Mamake analia kila siku na hata kwa sasa, hali yake ya kiafya si nzuri. Mkaza mwanangu kila siku analia akitaka kujua ni wapi alipo mumewe. Mimi nifanye nini sasa,” akasema Mzee Ngome.

Bw Hussein alisema tukio hilo la kumkamata jamaa huyo kisha baadaye familia kunyamaza ni kero kubwa kwa familia.

Alitaka familia hiyo ipate haki kwa kujua ni wapi alipo mpendwa wao.

“Tunajua kuwa Rais Magufuli ni Rais anayetenda kazi kwa haraka na hilo tunataka alitekeleze. Hata kama kijana huyo anazuiliwa kwa kosa fulani, familia ipo na haja ya kujua ni wapi alipo,” akasema.

Vile vile tunaumomba Rais Uhuru Kenyatta kuangalia suala hili kwa sababu huyu ni mkenya ambaye amekamatwa na anazuiliwa katika taifa jirani huku familia yake ikiwa haina habari kumhusu,” akaongeza.

Mke wa muathiriwa Bi Zaitun alisema kuwa walioana mwezi wa Machi mwaka huu na amamjua mumewe kama mtu mwenye bidi.

“Mimi sasa niko mja-mzito na mume wangu amekuwa tu karibu na mimi. Amekuwa wa msaada kwangu na ninaomba wale ambao wanamzuilia wafanye hima apatikane. Tunapitia hali ngumu sana kama familia,” akasema Bi Zaitun.