Uncategorized

Familia yamtaja Rex kuwa kijana mpole, mpenda amani aliyeangamizwa kikatili na polisi


MAANDAMANO ya amani ya kupinga Mswada wa Fedha 2024, 2024 mjini Nairobi wakati wa mchana uligeuka kuwa ya mauti baada ya polisi kumfyatua risasi kijana mmoja wa miaka 29.

Rex Kanyeki Masai, 29, alifariki Alhamisi jioni kutokana na majeraha aliyoyapata baada ya kupigwa risasi na polisi mwendo wa saa moja usiku.

Bi Gillian Munyao, mamake marehemu, alisema wana machungu sana huku akitaka haki itendeke.

“Nasikitika sana mwanangu kuuawa kwa njia kama hiyo. Kama familia, tunaomba haki itendeke,” akasema Bi Munyao akiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Nairobi City.

Bi Munyao alimtaja Rex kama kijana mpole na mpenda amani.

“Alikuwa ametoka kazini wakati alikutana na kifo chake. Rafiki yake alinieleza kuwa walipofika kwenye eneo la CBD karibu na National Archives, polisi walianza kurusha vitoa machazi kuwatawanya vijana waliokuwa wakiandamana,”

“Walianza kukimbia na polisi walikuwa wakiwafuata na kwa bahati mbaya risasi ikampata. Rafiki yake alijaribu kadri awezalo kumpeleka katika hospitali karibu ila akaaga pindi tu walipofika hospitalini,”

“Rex ni kifunguamimba wangu. Nimempoteza kijana mashuhuri sana,” akaongeza huku akilengwa na machozi.

Wanasiasa kama vile Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna ni miongoni mwa watu waliokuja kuifariji familia ya mwathiriwa.

Alisema hakuna haja polisi kutumia nguvu kuwatawanya vijana waliokuwa wakiandamana kwa amani.

Upasuaji wa maiti umeonyesha kuwa kijana huyo alipoteza damu nyingi baada ya kupigwa risasi mapajani.

Mwili wake umehifadhiwa Lee Funeral Home.

Naye Bw Chrispine Munyao, babake Masai, alisema mwanawe alikuwa kijana mpole na mcheshi.

“Rex alikuwa tegemeo letu. Ni kijana mchapa kazi sana.”

Mashirika ya kutetea haki za binadamu siku ya Ijumaa yaliibua wasiwasi kuhusu mienendo ya polisi wakati wa maandamano.

Jijini Nairobi pekee, Shirika la Amnesty International, katika ripoti yake lilisema kuwa zaidi ya watu 200 walipata majeraha, na wengine 50 walipelekwa kwa matibabu maalum.

Majeraha hayo yalitokana na majeraha ya tishu laini na kuvuta pumzi ya gesi ya kutoa machozi, kulingana na ripoti iliyotolewa saa kumi na mbili jioni.

Takriban maeneo 19 kote nchini yalishuhudia maandamano huku vijana nchini wakijitokeza kwa wingi kuelezea kukerwa kwao na Mswada wa Fedha wa 2024.

Maandamano hayo yalifanyika Nyeri, Nakuru, Kisumu, Uasin Gishu (Eldoret), Isiolo, Kisii, Laikipia (Nanyuki), Kilifi, Garissa, Kiambu (Thika), Kakamega, Nairobi, Meru, Kericho, Kirinyaga, Mombasa, Embu, Machakos. na Migori.

Wakati wa usiku, takriban watu 35 walikuwa wamekamatwa kote nchini, ripoti zilionyesha.

Ripoti ya pamoja ya Chama cha Wanasheria nchini, Chama cha Madaktari nchini, Muungano wa Watetezi, Kitengo Huru cha Kisheria cha Kimatibabu na Amnesty International ilibainisha kuwa waandamanaji walikuwa “wakiandamana kwa amani”.

“Tunawapongeza maelfu kadhaa ya waandamanaji, ambao wengi wao ni vijana, kwa kuandamana kwa amani, kuonyesha utulivu na adabu licha ya uchochezi wa polisi ambao walitumia nguvu kuwatawanya.”