Habari za Kitaifa

Familia yaomba msaada kuzika jamaa walioangamia Shakahola  

March 26th, 2024 2 min read

NA WACHIRA MWANGI

MWANAMUME aliyepoteza jamaa zake wanne katika mauaji yaliyotokana na itikadi kali yaliyohusishwa na mhubiri Paul Mackenzie Shakahola, Kilifi, anaiomba serikali kumsaidia kuwazika.

Miili ya jamaa hao ilitambuliwa kupitia vipimo vya msimbojeni – DNA.

Akizungumza na Taifa Dijitali, Bw Titus Ngonyo alielezea huzuni ya familia wanapojiandaa kupokea miili hiyo, ambayo imekuwa ikizuiliwa na serikali tangu ilipofukuliwa kutoka msitu wa Shakahola mwishoni mwa Aprili 2023.

“Tumezidiwa, tuna mawazo mengi na tumeamua kuzika wanne hao kwenye kaburi la pamoja nyumbani kwetu. Hata hivyo, tunahitaji msaada wa haraka kutoka kwa Serikali kwani hatuna rasilimali hata za kununua jeneza moja, sembuse hayo manne,” Bw Ngonyo alisema.

Japo watu wanne wa familia yake walioangamia katika janga la Shakahola, mjukuu mmoja, Ephraim, alinusurika mwaka jana.

Familia imepitia hasara kubwa, ikiwa ni pamoja na mke wa Bw Ngonyo, mwana Harry, mkwewe Emily Wanje, na mjukuu Seth Ngala, mwenye umri wa miaka mitano.

Alieleza juhudi zake zilizogonga mwamba kumshawishi mkewe asijiunge na kanisa la Good News International Church.

Majonzi yake yalizidishwa na kutotoka kwa mwanawe Isaac Ngala, aliyehepa kazi Nairobi mwaka 2019 kufuata mhubiri Mackenzie.

Mke wa Isaac, Emily, pia alijiuzulu kazi yake ya kufundisha Malindi ili kujiunga naye.

Licha ya huzuni yao, familia haijaweza kufanya mipango ya mazishi kutokana na onyo kutoka kwa mamlaka zinazohusika katika uchunguzi wa Shakahola, ambapo zilitahadharisha dhidi ya maamuzi ya mapema wakati wa mchakato wa kutambua miili ukiendelea.

William Ponda Titus, mwana wa pekee wa Bw Ngonyo aliyenusurika, alifaulu kukwepa janga hilo kwa kufanya kazi kama dereva Mombasa.

Kufuatia kutolewa kwa miili hiyo mnamo Machi 26, 2024 familia inakabiliwa na jukumu kubwa la kuhifadhi miili hiyo huku wakikusanya pesa kuwapa wapendwa wao mazishi ya heshima.

“Imekuwa safari ndefu. Angalau, nitakuwa nao karibu. Tunapanga kuwazika kwenye kaburi la pamoja karibu na nyumba yangu,” Bw Ngonyo alifafanua.

Wiki iliyopita, Mwanapatholojia mkuu wa Serikali Johansen Oduor alifichua kwamba kati ya waathiriwa 429 ambao miili ilifukuliwa msituni Shakahola, ni 34 pekee iliyotambuliwa.

Dkt Oduor alitangaza kwamba familia zitawajibika kushughulikia mazishi binafsi, bila kusaidiwa zaidi na serikali.

Familia ya Ngonyo, pamoja na nyingine nyingi zilizoathiriwa na janga la Shakahola, inatafuta usaidizi, kilio chao cha msaada kikisisitiza jinsi janga hilo lilivyoumiza maisha yao.