Kimataifa

Familia yasema Mkapa alifariki kutokana na mshtuko wa moyo

July 27th, 2020 1 min read

Na THE CITIZEN

FAMILIA ya aliyekuwa Rais wa Tanzania, Benjamin Mkapa, Jumapili ilisema marehemu alifariki kutokana na mshtuko wa moyo.

Kwenye misa ya wafu iliyofanyika katika Uwanja wa Michezo wa Uhuru, jijini Dar es Salaam, msemaji wa familia, William Erio, alisema Mkapa alipata mshtuko wakati akiendelea kupokea matibabu hospitalini.

Akiwahutubia maelfu ya watu waliofika kwenye hafla hiyo, alisema Mkapa alilalamika kuhusu maumivu Jumatano iliyopita ambapo alipelekwa hospitalini na kubainika alikuwa akiugua malaria.

“Alilazwa siku iyo hiyo na kuanza kupokea matibabu. Hali yake ya afya ilionekana kuimarika Alhamisi,” akasema.

Alieleza alimtembelea marehemu hospitalini siku iyo hiyo pamoja na baadhi ya jamaa zake, lakini wakaondoka baadaye.

“Nilikuwa naye Alhamisi. Alinipa ujumbe kumfikishia Askofu Alfred Nzigilwa kwamba hangeweza kuhudhuria hafla ya kumuaga kutokana na hali yake ya afya,” akaongeza.