Habari Mseto

Familia za walioangamia ajalini Kericho zadai fedha zao

November 1st, 2018 2 min read

Na SHABAN MAKOKHA

FAMILIA za watu 58 waliokufa katika ajali iliyotokea eneo la Fort Ternan Jumatano walikongamana nje ya afisi za kaunti ya Kakamega wakidai pesa zilizochangwa kufadhili mazishi ya wapendwa wao.

Pesa hizo zilichangwa wakati wa ibada ya wafu iliyofanywa katika uwanja wa Amalemba mjini Kakamega.

Familia saba ziliwapoteza wapendwa wao 11 wakati wa ajali hiyo iliyotokea Oktobs 10 katika eneo la Londiani kaunti ya Kericho.

Zinadai hazijakabidhiwa zaidi ya Sh7 milioni zilizochangwa wakati wa ibada hiyo ya wafu. Rais Uhuru Kenyatta alitoa Sh2.5 milioni, naibu wake William Ruto akatumana Sh500,000.

Wengine waliotoa michango kufadhili mazishi ni kiongozi wa chama cha Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi Sh100,000, aliyekuwa Seneta wa Kakamega Boni Khalwale Sh200,000, Seneta wa Bungoma Sh100,000, Seneta wa Kakamega Cleophas Malala Sh250,000, Mbunge mwakilishi wa kinamama kaunti ya Kakamega Elsie Muhanda Sh100,000 miongoni mwa wengine.

Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya alisema kaunti yake ilipoteza idadi kubwa ya watu katika ajali hiyo.

“Rekodi zaonyesha watu 37 kati ya wale 58 walifariki wanatoka kaunti ya Kakamega. Wawili walipelekwa mochari iliyoko hospitali ya St Marys eneo la Mumias, maiti moja ilipelekwa Yala na miili mingine 34 ilifadhiwa katika mochari iliyoko hospitali kuu ya Kakamega,” alisema Bw Oparanya.

Alisema kaunti yake ililipa gharama za mochari, kutoa masanduku ya kuwazika waliofariki pamoja na kutoa usafiri kwa familia na walioaga kutoka uwanja wa Amalemba hadi manyumbani mwao.

Familia moja kutoka Navakholo iliwapoteza watu sita waliokuwa wakirudi nyumbani ili kumzika nyanya yao.

Gavana wa Kericho, Dkt Paul Chepkwony, alisema serikali ya kaunti yake ililipa gharama za mochari na matibabu kabla ya miili kupewa familia zao wakazike.

Lakini familia hizo zikiongozwa na Bw Joshua Luseno, zilidai zilipewa Sh50,000 kutoka kwa mamlaka ya kushughulikia mikasa na Sh50,000 kutoka kaunti ya Kakamega.

“Pesa tunazodai ni zile zilitolewa na wahisani wakati wa sala kwa wafu.Pesa hizi zilikuwa sadaka na kamwe hazipasi kuwekwa katika akaunti,” alisema Luseno.

Naye Bw Adrian Makatu alidai magunia 78 ya mahindi aliyoyatoa Bw Ruto hayajawahi fikia familia zilizoathiriwa.