Familia za waliokufa kwenye mauaji ya Wagalla zataka fidia

Familia za waliokufa kwenye mauaji ya Wagalla zataka fidia

NA RICHARD MUNGUTI

FAMILIA za watu waliouawa kinyama miaka 38 iliyopita katika eneo la Wagalla na maafisa wa usalama zimeishtaki serikali zikiomba zilipiwe fidia.

Hata hivyo, kesi hiyo iliyokuwa imeorodheshwa kusikizwa na Jaji Hedwiq Ong’udi haikuendelea Ijumaa kwa kuwa wakili mkongwe na mwenye tajriba ya kesi kama hizi, Dkt John Khaminwa aliomba apewe muda kutafuta ushahidi zaidi kuhusu kesi hiyo.

Dkt Khaminwa anayewakilisha Kituo cha Sheria aliomba korti impe muda kupata ushauri zaidi na pia kufanya utafiti wa kina kuhusu kesi hiyo.

Alisema Dkt Khaminwa: “Ninaomba nipewe muda zaidi kusaka ushahidi wa kina kuhusu mauaji haya ya kinyama ya mwaka wa 1984. Wahasiriwa waliuawa kinyama pasi makosa.Wahasiriwa walikusanywa katika uwanja na kumiminiwa risasi na maafisa wa usalama.”

Dkt Khaminwa na wakili Assa Nyakundi walieleza Jaji Ong’udi kuwa wangependa wapewe ripoti ya dhuluma ya TJRC iliyogharimu serikali mamilioni ya pesa kuandaliwa.

“Tunaomba ripoti ya TJRC iwasilishwe kortini iwe ushahidi katika kesi hii,” alisema Nyakundi.

Mwanasheria mkuu aliyeshtakiwa kwa niamba ya serikali alikuwa na shahidi mmoja lakini kesi haikuendelea.

Mahakama iliamuru shahidi huyo arudi kortini Januari 20, 2023 kutoa ushahidi.

Aden ameeleza katika ushahidi baba yake aliyekuwa seneta wa kwanza eneo hilo la kaskazini mashariki aliuawa wakati wa tukio hilo.

“Hatujawahi ona maiti ya baba yangu ama kaburi lake. Tunaomba haki ifanyike,” Aden aliambia Taifa Leo katika Mahakama Kuu ya Milimani kesi ilipoahirishwa.

Aden anaomba Mahakama Kuu iamuru serikali iwalipe fidia.

  • Tags

You can share this post!

Wajawazito 550 hufa kila mwaka wakijifungua Kilifi –...

Kebs yapiga marufuku aina 10 za mafuta ya kupikia nchini

T L