Familia zaanza kuhama kutoka Mto Ngong

Familia zaanza kuhama kutoka Mto Ngong

NA SAMMY KIMATU

 

MAMIA ya wakazi waliokodi nyumba zao karibu na mto Ngong katika mitaa kadhaa ya mabanda ilioko kaunti ndogo ya Starehe wameanza kuhama kutafuta makao kwingineko.

Wakazi hao wanahofia kubomolewa kwa nyumba zilizo karibu na mto huo baada ya serikali kuweka alama ya kuonyesha sehemu inayofaa kuwa njia ya mto maarufu riparian land.

Akiongea na Taifa Leo jana, chifu wa eneo la Landi Mawe, Bw Mulandi Kikuvi alisema tayari serikali imeweka vikingi vya kuonyesha ardhi ya mto ya upana wa mita 10 kutoka kwa mto Ngong kila upande.

Aliongeza kwamba alama hizo ziliwekwa kuanzia daraja ya Express Kenya kutoka barabara ya Likoni kwenye Eneo la Viwanda kuelekea maeneo ya juu inalengwa kuelekea hadi kufikia mtaa wa mabanda wa Kibera.

‘’Serikali inataka kuokoa mto Ngong ndiposa maafisa wake wanapima mita kumi kutoka kila upande wa mto ili walio na nyumba zao karibu na mto waondoke mapema kabla serikali haijaafikia hatua ya kuwafurusha kwa kubomoa nyumba na tingatinga,’’ Bw Kikuvi asema.

Wiki jana, maafisa kutoka Mamlaka ya Kusimamia Rasilimali ya Maji (WARMA) ilipima na kuweka vikingi mitaani.

Hata hivyo, watu wasiojulikana walidaiwa kung’oa vikingi vyote usiku. Fauka ya hayo, chifu Mulandi alisema kung’oa vikingi ni kazi ya bure kwani serikali ina kifaa aina ya GPRS cha kutambua kulikowekwa alama.

Kwa mujibu wa ripoti ya Mradi wa Kukarabati Mto Nairobi, Mto Ngong na Mto Mathare, mito hiyo imechafuliwa na ardhi yake kunyakuliwa.

Ikiwa serikali itatekeleza mpango wa kuondoa walionyakua ardhi kwenye kingo za mito hiyo, maelfu ya watu watabakia bila makao.

Kufuatia hatua hiyo, mamia ya watu waliokodi nyumba kwenye maeneo yaliyoathirika wameanza kuondoka kwa hiari kutafuta makao kwingineko wasije wakapata hasara ikiwa nyumba zitabomolewa wangali hawajahama.

Inadaiwa kwamba baadhi ya mabwanyenye waliojenga nyumba za mawe wanaoathirika wameanza kuuzia wengine nyumba ambao ni wageni mitaani na hawajui lolote kuhusu mchakato huo.

“Wale hawajui kwamba wanauziwa nyumba zilizojengwa kwa ardhi ya serikali watajuta baadaye kwani hawajui wanauziwa nyumba na wamiliki wa hizi nyumba kwa sababu gani,’’ chifu Mulandi akadokeza.

Mto Ngong uliangaziwa na gazeti la Taifa Leo, runinga ya NTV sawia na gazeti la Daily Nation kwa kuwa una sumu baada ya makampuni kuelekeza maji yaliyo na kemikali hatari kutoka viwandani hadi ndani ya mto huo.

Vilevile, serikali nayo imepata wakazi katika mitaa ya mabanda wamejenga vyoo vyao karibu na mto na kuelekeza kinyesi ndani ya mto pia.

“Vyoo vyote mitaani ya mabanda vimeelekezwa hadi ndani ya mto Ngong. Viwanda navyo vinawachilia maji machafu yaliyo na kemikali hatari kuelekezwa ndani ya mto na kuhatarisha maisha ya watu, wanyama na mimea kule mto unakoelekea kabla ya kuungana na mto Athi,’’ Ofisa mmoja wa utafiti wa masuala ya afya akasema huku akiomba asitajwe jina lake.

You can share this post!

Vijana wataka wapewe nafasi katika miradi ya ujenzi wa...

Zawadi ya basi kutoka kwa Ruto yazua utata Mlima Kenya