FAO yafanya majaribio ya mpango wa kudhibiti shughuli za ufugaji wa kuku Nairobi, Kiambu

FAO yafanya majaribio ya mpango wa kudhibiti shughuli za ufugaji wa kuku Nairobi, Kiambu

NA SAMMY WAWERU

SHIRIKA la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), limezindua mradi wa majaribio kudhibiti hatari zinazotokana na shughuli za ufugaji kuku.

Mpango huo utatekelezwa katika Kaunti ya Nairobi na Kiambu, ukilenga kushirikisha wafugaji 60 wa kuku wa nyama.

Aidha, wafugaji 40 wanatoka Kiambu na 20 Nairobi.

Huku sekta ya ufugaji kuku ikiandikisha kukua, shirika hilo linaonya kwamba endapo mikakati kabambe kuidhibiti haitawekwa huenda ikazua hatari ya afya ya umma, kufuatia mkurupuko wa maradhi ya mifugo yanayoweza kuambukizwa binadamu.

FAO inataja Salmonella kama ugonjwa sugu unaotokana na wanyama, na kuambukizwa binadamu kupitia chakula kilichotagusana na kinyesi cha ndege – kuku.

“Ufugaji wa kuku unaimarika kuwa mojawapo ya sekta kuu hasa maeneo ya mijini, hivyo basi tunapaswa kujiandaa kwa matokeo hatari yanayoweza kuchipuka,” Dkt Stephen Gikonyo, mtaalamu wa masuala ya mifugo FAO, akasema wakati wa uzinduzi wa mradi huo jijini Nairobi.

Shirika hilo linahamasisha mikakati ya usalama wakati wa uzalishaji bidhaa za kuku na uchinjaji.

Mikakati hiyo aidha inapendekeza kuku kufugwa katika mazingira salama na safi.

Vilevile, wakulima wanatakiwa kufuga kuku katika vizimba vinavyodhibitiwa, na watu wanaoruhusiwa kuingia kulowesha makanyigio yao kwenye dawa yenye kemikali kuua viini vinavyosababisha vijidudu na pia kuvalia mavazi maalum.

“Uchinjaji, utekelezwe katika vituo vilivyoafikia vigezo vya ngazi ya kimataifa. Wanaofanya shughuli hiyo wasiwe na maradhi yoyote hasa yale ya kuambukiza na wavalie mavazi maalum kuzuia kueneza vimelea vya magonjwa,” akashauri Dkt Gikonyo.

Kwa mujibu wa mapendekezo ya mpango huo wa majaribio, wafugaji wanapaswa kununua vifaranga kutoka kwa waanguaji waliosajiliwa au kujiandikisha na asasi husika.

“Isitoshe, wadhibiti idadi ya kuku kwenye makazi ili kupunguza mkurupuko wa maradhi na maenezi.”

Idadi ya watu nchini na ulimwenguni kwa jumla ikiendelea kuongezeka, mazao ya kuku yanatarajiwa kupanda mara dufu.

Maeneo ya mijini yanakumbatia ufugaji ili kuafikia mahitaji.

Mfugaji wa kuku katika Kaunti ya Kiambu. PICHA | SAMMY WAWERU

Kulingana na ripoti ya FAO 2018, ulaji wa nyama za kuku na mayai unapaniwa kugonga tani 92,000 na 245, 000 kufikia 2050.

Inakadiriwa kuku wapatao milioni 27 nchini Kenya huchinjiwa katika vituo ambavyo havijaidhinishwa, milioni 10 kati yao wakiuzwa bila kukaguliwa na maafisa wa tiba ya mifugo.

  • Tags

You can share this post!

Twaha Mbarak akutana na Origi Anfield baada ya Liverpool...

Kocha Ten Hag ateua wakufunzi watakaomsaidia kunoa kikosi...

T L