FAO yajikakamua kuchangisha fedha kuokoa kaunti 23 zinazokumbwa na ukame

FAO yajikakamua kuchangisha fedha kuokoa kaunti 23 zinazokumbwa na ukame

Na SAMMY WAWERU

MAMLAKA ya kitaifa kuangazia majanga (NDMA) imeelezea wasiwasi wake kuhusu kaunti kumi za maeneo kame (ASAL) zinazoendelea kukumbwa na janga hatari la ukame.

Zinajumuisha Garissa, Isiolo, Kilifi, Kitui, Mandera, Marsabit, Samburu, Tana River, Turkana na Wajir, na kulingana na NDMA zinahitaji msaada wa dharura.

Mamlaka hiyo pia inaonya kwamba kaunti za Baringo, Kajiado, Kwale, Laikipia, Lamu, Makueni, Meru, Taita Taveta, Tharaka Nithi na West Pokot, ambazo zinashuhudia ukame wa kadri huenda mambo yakawa mabaya zaidi endapo hatua hazitachukuliwa.

Kwa mujibu wa data ya Idara ya Hali ya Anga Nchini na NDMA, mvua ya 2020 na ya mwaka huu, 2021 ilikuwa haba na ambayo ilisababisha kuwepo kwa hali inayoshuhudiwa katika kaunti hizo 23.

Idara ya utabiri wa hali ya anga inasema 2020 Kenya ilipokea kiwango cha chini cha mvua.

Februari 2020, NDMA ilidokeza kwamba watu milioni 1.4 katika kaunti hizo wako katika hatari ya upungufu na ukosefu wa chakula.

Hali hiyo ilichangiwa na kiwango cha chini cha mvua iliyopokewa kati ya mwezi wa Machi na Mei 2021.

Kufikia Juni, kaunti 12 kati ya 23 za maeneo kame zilikuwa zimekumbwa na ukame.

Huku mabadiliko ya tabianchi yakitajwa kuchangia kiangazi na ukame, serikali inajikakamua kuangazia hali, ikibuni kikosi maalum cha pamoja kutathmini mambo yalivyo na kuchukua hatua za dharura.

“Tumeweka mikakati kuchukua hatua zifaazo,” akasema Waziri wa Ugatuzi, Bw Eugene Wamalwa katika hafla iliyoandaliwa jijini Nairobi na iliyolenga kuchangisha fedha za shughuli hiyo.

Waziri aidha alisema kikosi kilichoundwa kimewajibika kuibuka na mwongozo wa hatua za dharura na mikakati ya kudumu ili kuokoa jamii za maeneo kame.

Serikali inahitaji kima cha Sh9.5 bilioni kuangazia ukosefu wa chakula kati ya Agosti na Desemba 2021 katika kaunti hizo 23.

Tayari muungano wa Bara Uropa (EU) umetoa mchango wa Sh547, 750, 000. Aidha, fedha hizo zinalenga kusambaza maji maeneo yaliyoathirika.

Wizara ya Ugatuzi inashirikiana na Shirika la Chakula na Kilimo (FAO – UN) kuokoa kaunti zilizotajwa kukumbwa na ukame.

Julai mwaka huu, FAO ilitia saini mkataba wa makubaliana na wizara kuweka mikakati kabambe na faafu kutafuta suluhu ya jamii zilizoathirika.

Mikakati hiyo inashirikisha kaunti zote kame, 23.

FAO hata hivyo inaomba ufadhili kutoka kwa wasamaria wema kujaza pengo la Sh2.3 bilioni zinazohitajika kuangazia ukame unaoendelea kushuhudiwa nchini.

“Lengo la FAO ni kuhakikisha taifa hili lina usalama wa chakula na pia kuboresha sekta ya kilimo hasa kwa kulenga wenye mapato ya chini na ndio maana tunashirikiana na serikali ya Kenya. Tunaomba wasamaria wema kushirikiana nasi katika hii safari,” akasema Carla Mucavi, mwakilishi wa FAO nchini Kenya.

Taifa hili limeshuhudia majangahai kadha katika siku za hivi karibuni, yakiwemo kero ya nzige, janga la Covid-19 na upungufu wa mvua.

Yamechangia kuwepo kwa uhaba wa malisho ya mifugo na chakula cha binadamu kaunti zilizoathirika.

Inakadiriwa watu milioni 2 wanahitaji msaada wa dharura wa chakula na maji katika kaunti hizo.

Jamii zinazoishi kaunti hizo zinategemea ufugaji; ng’ombe, mbuzi na ngamia, na ukame unaoshuhudiwa unawaathiri moja kwa moja, kufuatia wanyama wao kufariki.

Huku serikali ikiendelea kuweka mikakati maalum kuangazia mahangaiko ya maeneo hayo, ikiwemo kutenga ardhi kukuza nyasi na kutenga mifugo wakati wa kiangazi, Katibu katika Wizara ya Mifugo, Bw Harry Kimtai anasema unyakuzi wa mashamba unatatiza mipango hiyo.

Katibu katika Wizara ya Mifugo, Bw Harry Kimtai. Picha/ Sammy Waweru

“Licha ya kuwa tunajaribu tuwezavyo kuangazia matatizo ya kaunti kame, mashamba mengi ya serikali yamenyakuliwa hivyo basi kulemaza mikakati iliyopo,” Bw Kimtai akasema.

Aidha, alisema wizara yake imehusisha ile ya Mashamba katika mchakato mzima kurejesha vipande vya ardhi vya umma vilivyonyakuliwa.

You can share this post!

Guardiola kuagana na Man-City 2023 akimezea ukocha wa timu...

DNA yaonyesha mjukuu wa Moi ndiye baba ya watoto anaopinga...