Habari Mseto

Faraja kwa kampuni za wastani ERC ikitathmini ada za umeme

October 24th, 2018 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

TUME ya Kudhibiti Kawi (ERC) inamalizia kutathmini ada mpya ya umeme kwa kampuni za wastani na zile ndogo.

Kutokana na tathmini hiyo wenye kampuni hizo (SMEs) watakuwa wakilipa Sh21.95 kwa kilowati moja kwa saa (kWh) au asilimia 12.48 chini ya kiwango cha sasa cha Sh25.08 kwa  kilowati moja kwa saa (kWh).

Waziri wa Kawi Charles Keter alisema hatua hiyo inahitajika baada ya tathmini ya Agosti kwenda vibaya.

Wakati huo, biashara za SME ziliwekwa katika kiwango kimoja na wananchi wa mapato ya kadiri.

“Tunataka kuorodhesha SME katika kiwango kinachofaa kuambatana na agizo la rais kupunguza gharama ya umeme kwa wamiliki wa biashara. Baadhi yao waliwekwa katika kiwango cha maboma ambapo ada ya umeme ilipanda,” alisema Bw Keter.

Rais Kenyatta wiki jana aliagiza kupunguzwa kwa bei ya matumizi ya stima kwa wamiliki wa biashara ndogo ambazo huajiri asilimia 75 ya watu wote nchini kwa muda wa mwezi mmoja.