Habari Mseto

Faraja shuleni baada ya wanafunzi kuanzisha mradi wa bayogesi

July 21st, 2019 4 min read

NA RICHARD MAOSI

Ardhi iliyosheheni rutuba ndiyo maNdhari yaliyotukaribisha katika Kaunti ya Bomet, kilomita 22 kutoka mjini Kericho.

Ingawa wakazi wengi hapa ni wakulima na wafugaji, baadhi yao wamejiongezea ujuzi katika nyanja mbalimbli za kujiongezea kipato mbali na kilimo.

Wanafunzi wakionekana kutilia maanani swala la ukulima, katika hatua ya kuongeza nafasi za ajira siku za usoni, waje kuwa watu wa maana na kujitegemea.

Katika karne ya 21 uvumbuzi wa kisasa umekuja na faida nyingi kuliko hasara, wakulima na wajasiriamali wamefanikiwa kupiga hatua kubwa baada ya muda mfupi.

Mojawapo iliyotembelewa na Taifa Leo Dijitali ni Shule ya Upili ya Simoti  inayojivunia mradi wa kuzalisha bayogesi inayotumika kukidhi mahitaji ya wanafunzi 715 kwa mwaka.

Mwalimu Dennis Osano akionyesha mtama na wimbi unaokuzwa karibu ba mtambo wa kuandaa gesi inayotumika kwenye maabara ya shule. Picha/ Richard Maosi

Manufaa ya kutumia bayogesi

Ni bayana kuwa mradi wa kuzalisha bayogesi umesaidia kukata gharama ya kununua gesi kutoka kwenye viwanda kwa bei ghali ya Sh1,000 kwa kila mtungi wa kilo sita.

Kulingana na mwalimu mkuu Bw Charles Koech, hii ilikuwa ni njia mojawapo ya kusaidia shule ipate sehemu mwafaka ya kutupa samadi inayotokana na ng’ombe wawili wanaofugwa shuleni.

Vilevile Koech alieleza kuwa mradi wa kuzalisha biogesi kutokana na samadi, ungesaidia kutunza mazingira,na kupunguza uwezekano wa kukata miti kiholela kwa sababu ya kutafuta kuni.

“Wakazi wengi wa mashambani wanatumia kuni katika shughuli za kupikia,lakini tumejizatiti na kugundua njia mbadala na bora kuliko ile iliyozoeleka,”akasema.

Wanafunzi wakishirikiana kulisha mtambo wa biogesi kwa beseni iliyojaa samadi. Picha/ Richard Maosi

Gharama yake ni nafuu kwa sababu mkulima atahitaji samadi,paipu za kuunganisha mkondo wa gesi na nguvu kazi ya kuangalia mradi wenyewe katika kila hatua kabla ya bayogesi kuwa tayari kwa matumizi.

Mradi wenyewe ulianzishwa 2018 na shule ya Simoti ilitegemea kununua samadi kutoka kwa wakulima wadogo wanaowazunguka kabla ya kujipatia mifugo wao.

Kwa siku 365 shule ya Simoti haijakuwa ikinunua gesi kwa sababu wenyewe wamefanikiwa kuzalisha kiwango kinachoweza kutosheleza mahitaji ya kila siku ambayo ni kupikia na kwenye maabara.

Koech anasema shule inajipanga kuanzisha jikoni ya kisasa mwaka huu ili kuongeza jumla ya gasi inayozalishwa, iweze kutumika kuwapikia wanafunzi na kuwachemshia maji ya kuoga.

Mradi wenyewe unajumuisha usimamizi wa shule na wanafunzi ambapo kila mmoja amepatiwa jukumu la kutenda huku, wanafunzi wakionekana kuwa katika mstari wa mbele.

Muundo wa bayogesi ambapo samadi huchakachuliwa kabla ya gesi kutolewa. Picha/ Richard Maosi

Koech alisema mradi wenyewe utasaidia shule kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja na kuzuia matatizo kama vile moshi wa kuni onaoweza kuwaletea wanafunzi madhara ya kukohoa na maradhi ya pumu.

Koech aliongezea kuwa bayogesi huokoa muda kwa sababu huivisha chakula haraka na kuwapatia wanafunzi muda mwafaka wa kundelea na masomo yao badala ya kusubiri kuni,zinazochukua muda kupika.

“Ukiwa na nishati hii hauna haja ya kukata miti na mazingira yataishia kuwa salama zaidi ikizingatiwa kuwa watu watakuwa wakitegemea bayogesi,”mwalimu huyo mkuu aliongezea.

Matumizi ya mtambo

Wanafunzi wa shule ya Simoti wanatumia mtambo wa kawaida ambao ni tandarua,samadi,maji na beseni, lakini hili halifuti dhana kuwa wanapata nishati ya kutosha.

Mwalimu Koech aliongezea kuwa mkulima atahitaji takriban ng’ombe wawili kulisha muundo wake kwa samadi ya kutosha ambayo ni takriban kilo nne kila siku.

Wanafunzi wakilisha ng’ombe wawili wa shule wanaotumika kutoa samadi inayotumika kuzalisha bayogesi. Picha/ Rchard Maosi

Aidha mtayarishaji atahitajika kuupatia muundo wake muda baada ya kujenga ili upate kukomaa, na kishaye kumwagilia samadi kwa siku hamsini mtawalia bila kuutumia.

Hii itatoa nafasi kwa bakteria wanaopatikana ndani ya samadi kupata muda mwafaka wa kuzaana na kuchakachua samadi iliyoingia kabla ya kutoa pumzi hafifu za gesi na hatimaye biyogesi.

“Kwa kuzingatia ushauri wa kitaalamu mtumiaji hapaswi kutumia mtambo wake chini ya siku 45 kwa sababu bado gesi iliyozalishwa huwa haijatosha kuzalisha nishati,”alisema.

Hatua za kuchakachua samadi

Kwa mujibu wa mwalimu wa somo la zaraa Bw Dennis Osano anasema uzalishaji wa nishati ya bayogesi unahitaji teknolojia rahisi ambapo mkulima atasaka sehemu ya kuhifadhi samadi.

Mtayarishaji anaweza kutumia tanki kubwa au beseni ambapo samadi huchakachuliwa na bakteria wanaozaana kutokana na viini vya mamilioni ya bakteria wanaoongezeka.

Wakazi wengi hapa ni wakulima wa majani chai kwa hivyo wanategemea kuni kupika jambo linalohatarisha misitu. Picha/ Richard Maosi

Baada ya muda mfupi wa siku tano hivi matokeo yake huwa ni gesi pamoja na mbolea hai inayoweza kukuza mimea, katika shamba bila kutegemea zile za viwanda zenya madini ya phosphorus na ammonia.

Uzalishaji wa nishati ya kawi unahitaji sehemu tatu ambapo moja ni ya kumwaga samadi,pili ni sehemu ya kufanyia mchanganyiko wa maji na samadi na hatimaye chujio ya kuhakikisha gesi inayotolewa ni safi kwa matumizi .

Wanafunzi walitumia tandarua nyeusi,ili kufanikisha hali endelevu ya kuzalisha nishati rahisi ,kwanza ili kuimarisha joto katika muundo huu unaovuta miale ya jua kwa asilimia kubwa na kuharakisha uzalishaji wa kawi.

Uzalishaji wa nishati yenyewe unatemea kujaza samadi na kutoa fursa mwafaka ya kuchakachua samadi kabla ya kuzalisha kawi ambayo haishi kwa haraka kama aina nyingine za gesi zinazoweza kukatika njiani.

Osano anasema baada ya samadi kuchujwa inaweza kuruhusiwa kutoka nje ya muundo huu,na endapo itakingwa na kuhifadhiwa vizuri inaweza kutumika shambani kukuza mimea na ubora wake ni wa hali ya juu sana.

Mbolea inayotokana na samadi ndani ya bayogesi inavyotumika kukuza nyasi ya napier. Picha/ Richard Maosi

“Cha msingi ni kwa mkulima kuhakikisha analisha mtambo kwa samadi ya kutosha ili kupata gesi ya kutosha bila kukoma,ngombe wawili hivi wanatosha kufanikisha hili,”akasema.

Aliongezea kuwa ni muhimu mkulima kuhakikisha anatumia lishe sahihi ili kuhakikisha wanatoa samadi yenye ubora wa kipekee.

Samadi ya ubora wa kipekee inahitajika kuwa na mchanganyiko wa lishe ya nyasi za rangi ya kijani kibichi,lishe za viwandani na maji ya kutosha .Pia mkulima afanye juhudi kuwazuia mifugo wake wasile vitu vigumu kama mawe na karatasi zilizoshusha hadhi ya samadi.

Maoni ya wanafunzi

Japheth Koros mwanafunzi wa kidato cha nne anaungama kuwa uzalishaji wa bayogesi umemsaidia kuongeza upeo wa maarifa na imedhibitisha kuwa inaweza kuongeza rutuba katika udongo.

Aidha yeye pamoja na wenzake wamekuwa wakilisha mtambo huo kwa samadi mara mbili kila siku yaani asubuhi na jioni.

Anasema mtambo wa bayogesi umekuwa ukiwasaidia katika maabara ya kemia,fizikia na bayolojia kufanyia utafiti wa kisayansi.

“Ni mradi ambao mbali na kuboresha matokeo yetu shuleni, unatuandaa kwa mtihani wa kitaifa KCSE mwisho wa mwaka huu,” mwanafunzi huyo aliongezea.