FATAKI: Ajabu kuu ‘wife material’ kuwa mwanamke anayevumilia shida pekee!

FATAKI: Ajabu kuu ‘wife material’ kuwa mwanamke anayevumilia shida pekee!

NA PAULINE ONGAJI

BILA shaka umekumbana na lile neno “wife material” ambalo limekuwa likirushwa rushwa huku na kule hasa na madume.

Kwa madume wengi, wife material ni mwanamke atakayevumilia shida. Binti asiye na gharama. Hamnunulii mavazi, vipodozi wala kumgharimia nywele. Mwanamke anayejitwika majukumu yote ya kifedha nyumbani licha ya kuwa mume anafanya kazi na kwa upande wake hawajibiki, japo, kwa upande mwingine bibi huyo huyo anamburudisha na kummalizia ashiki.

Kwa hawa wanaume, wife material ni mwanamke anayevumilia maisha magumu na mateso. Binti ambaye chakula kitakosekana nyumbani kwa siku kadhaa lakini hatonung’unika wala kwenda popote.

Katika akili za madume hawa, mwanamke wa aina hii ni yule ambaye atafumbia macho tabia ya mwanamume kuwa na mahusiano mengi ya kando au hata kutoweka kwa siku kadhaa na kurejea bila maswali. Mwanamke anayekaa kimya huku mwanamume akiendelea kutafuna vimada mbali mbali mtaani kote.

Mwanamke asiyesema amechoka. Yaani mnatoka nyote kwenda kazini na kurejea jioni na hata wakati mwingine baada ya mume, ilhali akirejea anatarajiwa kumuandalia mwanamume chakula tena akiwa umepiga magoti.

Mwanamke anayejisahau pamoja na ndoto zake kwa wema wa mume na wanawe. Bila shaka kama mwanamke una wajibu wa kuilinda familia yako, lakini sio huku wewe mwenyewe ukijisahau.

Ikiwa wewe ni mmoja wa kati ya hizi au zote, fahamu kwamba hiyo sio kuwa mke mwema, bali ni utumwa. Ndoa haipaswi kuwa shubiri au mzigo kwa yeyote katika uhusiano huo. Nyote mnapaswa kufurahia maisha haya.

Zaidi ya yote, wale wanaopenda kutumia neno hili sana husahau kwamba kabla ya mwanamke awe mke mzuri lazima mazingira yamfae; lazima mwanamume awe ameunda mazingira mwafaka kwa mwanamke kuwa mzuri.

Mazingira haya ni uaminifu, heshima, mwanamume kuwajibika na kufanya mambo ambayo anapaswa kufanya kama kichwa cha nyumba. Katika jamii inayomtarajia mke kuwa malaika, sharti mazingira yawe ya mbinguni.

Hakuna jinsi ya kutarajia kuishi na malaika ilhali kuta za nyumba zinateketea sawa na jehanamu.

  • Tags

You can share this post!

DINI: Utavuna ulichopanda, hakuna mkato maishani!

WASIA WA NDOA: Utafanyaje ndoa ikikosa kuridhisha?

T L