Makala

FATAKI: Fisi si madume pekee, akina dada pia ni hatari kubwa!

March 9th, 2019 2 min read

Na PAULINE ONGAJI

SIJUI hili wazo la kwamba madume pekee ndio huwa na tabia ya ufisi wanapomuona binti hasa mrembo, lilitoka wapi.

Ikiwa wewe ni mpenzi wa muziki bila shaka una mazoea ya kila mara kusikiza nyimbo na hata kutazama video za wanamuziki tofauti.

Hasa kinachonifurahisha zaidi ni kutazama shoo za moja kwa moja, mubashara au ukipenda ‘live shows’ ambapo mashabiki wanapata fursa ya kukutana ana kwa ana na wanamuziki wanaowaenzi.

Ikiwa wewe ni mpenzi wa shoo za aina hii, basi bila shaka umeshuhudia tabia fulani ya kukera hasa miongoni mwa mabinti.

Hii tabia ya mashabiki wa kike kusukumana na hata kulia ili kunasa jicho la msanii wa kiume.

Sio siri kuwa wasichana huonekana kupumbazwa zaidi na wanamuziki wa kiume zaidi ya jinsi wa kiume wanavyoduwazwa na wasanii wa kike.

Utawaoana mabinti wakipiga mayowe huku wengine wakilia kana kwamba wamewapoteza wapendwa wao.

Jambo hili nimelishuhudia hata miongoni mwa baadhi ya wanamuziki mashuhuri wa kike wa humu nchini ambao mara kadha hudondokwa na mate pindi msanii wa kiume wa haiba ya juu kutoka ng’ambo anapozuru Kenya.

Sijui kama umepata fursa ya kutazama video fulani iliyoenea mtandaoni majuma kadha yaliyopita, na ambayo ilimuonyesha msanii wa RnB, R. Kelly akitumbuiza jukwaani ambapo anafanya sarakasi kana kwamba anachochea hisia za mahaba miongoni mwa akina dada waliomzingira.

Mashabiki wamfuta jasho

Msanii huyu anatoa ulimi nje huku mashabiki hawa wakionekana kumfuta jasho kwa utaratibu vilevile akiwapa fursa yao kumpapasa msamba.

Sio tu katika fani ya burudani, maeneo ya ajira pia hayajasazwa. Hapa unakumbana na akina dada au hata wanawake waliokomaa wakifanya kila wawezalo kunasa jicho la dume fulani.

Na huenda ulisikia kuhusu visa vya warembo waliokuwa wakimng’ang’ania msanii Diamond, kiasi cha kurushiana maneno makali, licha ya kujua angalau alikuwa ama ana mwanamke ambaye ‘ukuruba wake ni wa zaidi’.

Nakumbuka chapisho fulani mtandaoni lililodai kuwa mabinti kadha walikuwa wanamsaka msanii mmoja aliyesemekana kuwatunga mimba.

Kaka huyo alipohojiwa alisema kwamba akina dada hao walikuwa wakimuandama licha ya kujua kwamba ana mtu wake kimahaba.

Bila shaka Diamond wala msanii huyu hawaondolewi lawama lakini jambo ambalo nasisitiza ni kwamba hata kwa wanawake kuna ‘fisi ambao mawindo yao ni madume’.