Makala

FATAKI: Hivi vitisho vya pesa nane havitutetemeshi!

February 23rd, 2019 2 min read

Na PAULINE ONGAJI

HIVI majuzi kuliibuka habari za ajabu kutoka nchini Uganda.

Kulingana na taarifa za gazeti moja nchini humo, Wizara ya Utalii nchini Uganda ilikuwa inatangaza mabinti wanene kama mojawapo ya vivutio vya kunasa watalii nchini humo.

Nia yao ilikuwa kutangaza mabinti wenye makalio makubwa lakini kidogo walipotoka kwani wengi wa wanawake waliokuwa kwenye gwaride hilo walikuwa wanene huku, lakini hiyo ni mada ya wakati mwingine.

Nikirejea suala hilo, inadunisha kwamba wizara ya nchi hiyo inaona kwamba hakuna jambo muhimu ambalo mabinti wao wanaweza changia katika uchumi wao pasipo miili yao. Lakini pia, hiyo ni mada ya wakati mwingine.

Suala hili la wizara ya utalii nchini Uganda kuwaanika mabinti wanene kama vivutio vya kiutalii liliibua hisia tofauti mtandaoni ambapo nilikumbana na madume kadha wakijadili jinsi walivyokuwa wakipanga kwenda huko angaa pia wao kupata sehemu yao ya makalio hayo.

Pengine walikuwa wanasema hivyo huku nia yao ikiwa kubabaisha mabinti Wakenya, lakini ole wao kwani hii sio mara ya kwanza kwetu kukumbwa na vitisho vya aina hii.

Nakumbuka kulikuwa na mawimbi sawa na haya miaka kadha iliyopita ambapo mabinti kutoka taifa hilo walimiminiwa sifa kwa kuwa wanyenyekevu na wanyonge, kiasi cha kuwa nikiwa mdogo nilisimuliwa hadithi za baadhi ya madume waliokimbilia nchini humo kujinasia wake.

Kwa madume hao, ambao mbali na kuuabudiwa wangeandalia vyakula na kukaribishwa nyumbani wakiwa wamewapigia magoti. Nakumbuka enzi hizi kwani kuna jamaa yetu mmoja ambaye alikuwa mmoja wa hao madume waliokimbilia huko kupata wake.

Nakumbuka tukiwa wadogo tungemtembelea na kumuona bibi huyo akimnawisha mikono na kumuandalia chakula mezani akiwa amepiga magoti, utamaduni alioupitisha kwa kila mjakazi aliyekuja kwake kufanya kazi, na nusura atuambukize, ila mamangu na ujeuri wake alikataa katakata kukubali mabinti zake kukandamizwa.

Mambo yabadilika

Hata hivyo kufupisha hadithi hii, baada ya mwanamke huyo kuzaa wana kadha na kukumbana na uhalisi wa maisha ya ndoa, mambo yalibadilika.

Mazoea ya kulidekeza dume kama mfalme, halikumzuia kaka huyo kuoa wake wengine wawili Wakenya ambapo haikuwa muda kabla ya mapenzi na heshima hiyo kuisha, n ahata kaka huyo alipokuwa akikaribia kufa bibi alikuwa akimnyima chakula.

Kwa hivyo sawa na mwandishi fulani alivyosema wakati mmoja kwamba mawimbi yaliyowasukuma mabinti wa Kenya kwa madume kutoka Magharibi mwa Afrika yatatulia, hizo mbio za kuelekea nchini Uganda bila shaka zitafika ukingoni, na hayo yatakapojiri, sisi kama mabinti wa Kenya tutakuwa hapa tayari kuangua kicheko.