Makala

FATAKI: Hujafunga zipu yako lakini uko wa kwanza kukemea kina dada kwa ‘kugawa’

April 19th, 2019 2 min read

Na PAULINE ONGAJI

HUENDA umepata fursa ya kusikia mojawapo ya mahubiri ya mchungaji fulani kutoka Tanzania ambaye amekuwa akivutia hadhara hasa mtandaoni kutokana na fataki anazoangusha.

Mada zake hasa huhusisha masuala ya kawaida katika jamii ambapo mara kadha amekuwa akigusia masuala ya mapenzi na mahusiano.

Hasa nakumbuka video yake moja iliyokuwa ikisambaa kwenye mtandao wa kijamii ambapo alikuwa akiwafokea wanaume wanaosisitiza kwamba hawawezi kuwaoa warembo ambao tayari wana watoto au wale ambao sio mabikira.

Mhubiri huyu aliwafokea madume hawa huku akiwaelekezea kidole kwa kujigamba jinsi wanavyojifanya kutotaka mabinti ambao ‘wametumika’ ilhali wao wenyewe ni sawa na ganda la mua.

“Nataka msichana ambaye hajazaa… Ungekuwa unapata mimba ungekuwa umepata ngapi? Umewapa mabinti wangapi mimba? Wewe used na unataka kitu kipya?” alisema huku waumini wakiangua kicheko.

Ni hoja ninayokubaliana nayo asilimia moja kwa mia moja kwani ukiangalia wanaume wanaosisitiza eti lazima wapate kitu kipya, wengi wao wameramba ramba huku na kule na hata kupanda mbegu katika mashamba kadha.

Iwe vipi wewe umeshindwa kufunga zipu ya long’i ilhali wewe ni wa kwanza kutusi mabinti walio na mazoea ya kuteremsha bendera?

Ni hoja niliyoizungumzia miezi kadha iliyopita hasa kuhusiana na jamii na dini zinazosisitiza ubikira wa binti kabla ya kuolewa.

Niliuliza iwapo wahusika wanasisitiza kuwa lazima binti awe bikira wakati wa ndoa, je ubikira wa wanaume una umuhimu?

Ikiwa mko tayari kutudhihirishia kuwa huo usiku wa kwanza wa fungate kaka hakulitumia jembe lake kwingineko basi ana kila haki ya kusisitiza kwamba sharti mwanamke awe bikira.

Hii ni mojawapo ya sababu zinazonifanya kuzidi kumshabikia nyota wa muziki Diamond Platinumz, licha ya kukumbwa na kashfa mbali mbali za mapenzi.

Haina shaka kwamba bwana huyu ameng’aa kimuziki na kutikisa kila pembe sio tu nchini mwao au Afrika Mashariki, bali bara lote la Afrika. Lakini ufanisi wake haukumzuia kumchumbia na hata kumuoa mkewe wa zamani Zari Hassan, ambaye wakati huo tayari alikuwa mke wa mtu na mama wa watoto kadhaa.

Japo waliachana, wakiwa pamoja, kaka huyu alionekana kumuenzi binti huyo na hata mara kwa mara kumzawadi tunu za bei ghali. Hii ilidhihirisha kwamba yeye ni mmoja wa madume wenye mawazo mapana kwani anaelewa kwamba thamani ya binti haipimwi kwa ubikira au iwapo ameangusha watoto kadhaa au la.

Na wale wanaotumia masuala haya kama mizani ya kutambua thamani ya binti wanapaswa kujiuliza iwapo ingetumika pia kwa wanaume ni wangapi wangeupita mtihani huu?