Michezo

Fataki kulipuka Posta Rangers na Nairobi Stima zikiwania fursa ligini

June 19th, 2019 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

KOCHA John Kamau wa Posta Rangers amewataka wachezaji wake kuzamisha chombo cha Nairobi Stima kwa mara nyingine hii leo Jumatano na kujipa uhakika wa kuendelea kushiriki kivumbi cha KPL msimu ujao.

Rangers wanashuka ugani Kenyatta, Machakos kwa mechi ya marudiano wakijivunia ushindi wa 2-1 katika mchuano wa mkondo wa kwanza uliosakatwa wikendi jana mjini Naivasha.

Katika kipute hicho, mabao ya Rangers yalipatikana kupitia kwa Joackins Atudo na Francis Nambute. Goli la Stima lilipachikwa wavuni na Dennis Oalo ambaye anajivunia jumla ya mabao 26 kapuni mwake kufikia sasa.

“Ilivyo, sioni lolote litakalowazuia vijana wangu kuendeleza ubabe wao dhidi ya Stima. Kikosi kinatawaliwa na hamasa tele na kubwa zaidi katika maazimio yao ni kusalia katika KPL msimu ujao,” akasema Kamau.

Historia

Historia ni jambo jingine linalotazamiwa kuchangia motisha ya Rangers hasa ikizingatiwa kwamba hakuna kikosi cha Ligi ya Supa (NSL) ambacho kimewahi kufuzu kwa gozi la KPL kupitia mchujo.

Hii ni mara ya pili kwa vikosi kukutana kuwania nafasi ya kufuzu kwa kivumbi cha KPL.

Thika United waliwahi kukutana na Ushuru FC ya NSL na kufanikiwa kusajili ushindi wa jumla wa 2-1.

Rangers walikamilisha kampeni za KPL msimu huu katika nafasi ya 16 kati ya timu 18, huku Stima wakiambulia nafasi ya tatu katika NSL nyuma ya Kisumu All Stars na Wazito ambao walifuzu moja kwa moja kuingia KPL msimu ujao.

Stima walipoteza mechi mbili pekee kati ya 38 za NSL na wakajizolea alama 80, sawa na Kisumu All Stars waliowapiku kwa wingi wa mabao.