Michezo

Fataki kulipuka Senegal na Algeria wakipapurana

June 27th, 2019 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

FATAKI zinatarajiwa kulipuka leo jijini Cairo wakati Senegal watakapochuana na Algeria katika mechi ya pili ya Kundi C kwenye fainali za Kombe la Afrika (AFCON).

Mshindi wa mchuano huo unaotazamiwa kutawaliwa na kasi zaidi na wingi wa hisia, atajikatia tiketi ya kuingia awamu ya mwondoano wa fainali za mwaka huu zinazoendelea nchini Misri.

Senegal wanaoorodheshwa wa kwanza barani Afrika, waliwahi kukutana na Algeria katika hatua ya makundi ya AFCON na kuambulia sare tasa kwenye fainali zilizoandaliwa nchini Gabon mnamo 2017.

Licha ya Senegal kukosa huduma za mvamizi matata wa Liverpool Sadio Mane katika mchuano wao wa ufunguzi wa Kundi C dhidi ya Tanzania mnamo Jumapili, kikosi hicho cha kocha Aliou Cisse kilisajili ushindi wa 2-0 kirahisi.

Kulingana na Cisse, uspesheli katika mchuano huu ni jinsi ambavyo vijana wake walivyopania kuchukulia kivumbi chenyewe kama fainali.

Katika kipute kingine cha leo Alhamisi, Madagascar walioambulia sare ya 2-2 dhidi ya Guinea katika mchuano wa ufunguzi wa Kundi B watavaana na Burundi.

Burundi watapania kujinyanyua baada ya kuzabwa 1-0 na Nigeria katika dakika za mwisho mnamo Jumamosi.

Fowadi mahiri wa Inter Milan, Keita Balde aliwafungulia Senegal ukurasa wa mabao kunako dakika ya 28 huku kiungo Krepin Diatta wa Club Brugge akizamisha kabisa chombo cha Tanzania ambao leo watapimana ubabe na Kenya katika gozi kali. Senegal waliotamalaki mchezo huo na kuwazidi wapinzani wao maarifa katika kila idara, walielekeza makombora 24 langoni pa Tanzania ambao kwa sasa wameapa kuwateketeza Kenya katika mechi yao ya pili.

Japo hawajawahi kunyanyua ufalme wa AFCON, Senegal wanaorodheshwa na FIFA katika nafasi ya 22 duniani, na wana kila sababu ya kutawala kampeni za mwaka huu. Kwa upande wao, Algeria wanashikilia nafasi ya 12 barani Afrika na wanaorodheshwa wa 68 duniani.

Kikosi hicho kilitinga fainali ya AFCON kwa mara ya mwisho mnamo 2002 na kikazidiwa maarifa na Cameroon kwa kichapo cha 3-2 kupitia penalti baada ya kuambulia sare tasa mwishoni mwa dakika 120.

Mbali na Mane, masogora wengine wanaotazamiwa kuibeba Senegal mabegani ni Idrissa Gueye wa Everton, nahodha Cheikhou Kouyate wa Crystal Palace na beki Kalidou Koulibaly wa Napoli SC ambaye kwa sasa anahusishwa pakubwa na uwezekano wa kutua ugani Old Trafford kuvalia jezi za Manchester United.

Kwa upande wao, Algeria watajibwaga pia ugani wakijivunia hamasa tele baada ya kuwapepeta Kenya 2-0 mnamo Jumapili.

Baghdad Bounedjah aliwafungia Algeria almaarufu ‘Desert Foxes’ mkwaju wa penalti kunako dakika ya 34 kabla ya kiungo matata wa Manchester City, Riyad Mahrez kuongeza la pili mwishoni mwa kipindi cha kwanza. Licha ya kutokuwa nyota tegemeo kambini mwa Algeria katika fainali za 2017, Mahrez kwa sasa ni mhimili mkubwa wa kikosi hicho ambacho kimemwaminia unahodha.

Zaidi ya Mahrez na Bounedjah ambaye aliwafungia Al-Sadd kutoka Qatar jumla ya mabao 39 katika kampeni za Ligi Kuu ya taifa hilo msimu huu, wachezaji wengine ambao wanatarajiwa kukitambisha zaidi kikosi cha Algeria ni kiungo Sofiane Feghouli wa Galatasaray na Yacine Brahimi ambaye kwa sasa huvalia jezi za FC Porto nchini Ureno.

Kufikia sasa, Algeria wanaselelea kileleni mwa Kundi C kwa alama tatu sawa na Senegal ambao kwa pamoja na Nigeria, Misri, Ghana na Morocco, wanapigiwa upatu wa kunyanyua ufalme wa taji la AFCON mwaka 2019.

Senegal na Misri ambao wanashikilia nambari nane barani Afrika, ni kati ya timu sita ambazo zilitiwa katika tapo la kwanza wakati wa droo ya makundi ya AFCON 2019 kwa sababu ya ubora wa nafasi zao katika orodha ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA).

Vikosi vingine katika tapo hilo la kwanza ni Morocco (4), Nigeria (3), Tunisia (2) na mabingwa watetezi, Cameroon (7). Kati ya vikosi vilivyotiwa katika tapo la pili, Ghana (6), Algeria (12) na Ivory Coast (11) vinatarajiwa kuwika zaidi kuliko DR Congo (5) na Afrika Kusini (14).