Makala

FATAKI: Lazima tuambiane ukweli hata kama unauma

September 7th, 2019 1 min read

Na PAULINE ONGAJI

NIKO katika kikundi kimoja cha mabinti kwenye WhatsApp ambapo juma lililopita, kulichipuka mjadala fulani wa kufurahisha.

Kuna binti aliyekuwa akilalama kuhusu jinsi siku hizi kutokana na msisitizo wa kupigania haki za wanawake, imekuwa hatia kukosoa chochote anachofanya mwanamke, hata iwapo ni kosa la wazi.

Hii ilinikumbusha mada fulani niliyozungumzia miezi kadha iliyopita kuhusu jinsi siku hizi imekuwa vigumu kutofautisha baina ya upumbavu na utetezi wa usawa wa kijinsia na hasa haki za wanawake.

Mambo huwa mabaya hata zaidi ikiwa ukosoaji huu unatoka kwa mwanamke. Katika himaya hii, haitakuwa rahisi kwako kutoa maoni yako makali na kuepuka pasipo kuitwa msaliti au kuambiwa kwamba una wivu.

Msimamo huu hasa utatoka kwa hao mabinti wanaoyafumbia macho mabaya yanayofanywa na wanawake kila siku, kwa kisingizio kwamba wanatetea jinsia ya kike.

Hiki ni kikundi cha wanawake wanaojidai kuwa watetezi wakali wa jinsia ya kike, huku wakiyafumbia macho maovu yanayotekelezwa na baadhi ya mabinti katika jamii.

Hii yanikumbusha kuhusu kikundi fulani cha mabinti wanaojidai kutaalumika, na ambao huwa mstari wa mbele kupaza sauti kusisitiza jinsi wanawake wanavyopaswa kutengewa nyadhifa za uongozi, ilhali wanajitia hamnazo, viongozi wa kike wanapohusishwa kwenye kashfa za wizi wa pesa za umma.

Lakini pengine hawapaswi kulaumiwa kwani wengine wako kazini huku marupurupu yao yakihesabiwa kuambatana na mara ngapi wamefungua kinywa kutetea jinsia hii kwa vyovyote.

Ili harakati za kuhakikisha usawa wa kijinsia zinaheshimiwa, jitihada hizi hazipaswi kuonekana kupendelea upande wowote. Ikiwa inasinya kwa mwanamume kuiba mali ya umma, tunapaswa kukerwa hata zaidi mwanamke anapohusika au hata kutajwa katika uhalifu huu, kwani hiyo ni hatua moja inayovuruga jitihada za kuhusishwa katika nafasi za uongozi.

Lakini hilo litaafikiwa vipi ikiwa ukweli hauelezeki tena eti kwa sababu tunahofia kuonekana kana kwamba tunaenda kinyume na jinsia ya kike au tuna wivu?